VIONGOZI WA MAZIWA MAKUU WATOA SIKU TATU KWA M-23 NA SERIKALI YA DRC KUREJEA KWENYE MEZA YA MAZUNGUMZO

 

Wapatanishi wa mgogoro wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoa muda wa siku tatu kwa waasi wa M23 na serikali ya nchi hiyo kurejea kwenye meza ya mazungumzo huko jijini Kampala Uganda.

Hayo ni baada ya kikao cha viongozi wa kanda ya maziwa makuu kiliyofanyika juzi huko kampala Uganda.

Kiongozi wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa amesema wao wapo tayari kwa mazungumzo na wajumbe wake wamewasili mjini Kampala kwa ajili ya mazungumzo hayo.

Bertrand Bisimwa amesema kundi lake limechukua uamuzi wa kurejea katika meza ya mazungumzo wakitekeleza wito huo wa mataifa yanayounda Kanda ya Maziwa Makuu kutaka mazungumzo kuendelea ndani ya siku tatu.

Mazungumzo hayo baina ya serikali ya DRC na kundi la waasi wa M23 yalianza tangu Desemba mwaka jana jijini Kampala lakini hadi sasa hayajafikia kwenye hatua ya kuridhisha.

Raisi wa Uganda Yoweri Museveni ambaye ni mwenyekiti wa mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu amesema kuwa kuna nafasi kubwa ya makubaliano kati ya pande hizo mbili.

Mazungumzo hayo baina ya serikali ya DRC na kundi la waasi wa m23 yatakuwa chini ya mpatanishi raisi wa Uganda Yoweri Museveni.

Hata hivyo wananchi wa DR Congo Wanaona kwamba mazungumzo hayo hayana tija yoyote bali suluhu ni M23 kuachana na mpango wao.


TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: