SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete
kuteua na kuapisha makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wapya na
makatibu tawala wa mikoa, wamekutana kujadili vipaumbele vya Serikali na
kupeana maelekezo.
Akizungumza katika mkutano huo jana,
Katibu Mtendaji, Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango,
alielezea umuhimu wa Serikali kuwa macho na baadhi ya wabunge
wafanyabiashara, ambao wamekuwa wakitetea hoja kwa maslahi binafsi.
Alitoa hadhari hiyo, huku akielezea kuwa
katika mazingira ya sasa, mwingiliano wa majukumu kati ya ngazi za
kiutendaji za Serikali na ngazi za kisiasa kama Bunge na Baraza la
Mawaziri vimeongezeka.
Alitolea mfano wa Kamati ya Bajeti ya
Bunge, ambayo alisema ina wajibu wa kubainisha vyanzo vya mapato, kazi
ambayo zamani ilikuwa ikifanywa na Serikali.
Pia Kamati hiyo, ina wajibu wa
kubainisha viwango vya kodi au tozo, viwango vya kukopa na ukomo wa
bajeti kwa dhana ya kuisimamia Serikali.
Alitaka maofisa masuuli kusimamia hatua
zote za mzunguko mpya wa bajeti katika maeneo yao: “Maofisa masuuli
mtambue nyakati zimebadilika, Bunge la sasa ni tofauti na la siku za
nyuma.
Ni muhimu maandalizi ya mipango na
bajeti yafanyike kwa weledi na kuzingatia ratiba.” Ili utekelezaji wa
miradi ya maendeleo uanze mapema, Dk Mpango alitaka maofisa hao
wakamilishe mapema mipangokazi na mtiririko wa rasilimali fedha kwa
ajili ya uchambuzi baada ya bajeti zao kupitishwa na Bunge.
Pia aliwataka kuzingatia sheria za fedha
na kuepuka kufanya uhamisho wa fedha tofauti na ilivyoidhinishwa na
Bunge, kwa kuwa hatua hizo zitaibua hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa
Hesabu za Serikali (CAG).
Aliwataka kupitia kwa umakini na
kuhakiki takwimu na taarifa zote za utekelezaji wa bajeti na miradi ya
maendeleo wanayoisimamia, kabla ya kuziwasilisha katika ngazi za
kisiasa, likiwamo Baraza la Mawaziri na Bunge.
Akifungua mkutano huo wa siku tatu,
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitaka washiriki kusimamia
vipaumbele vya Taifa, vya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Serikali ya
Wazi na Serikali mtandao.
“Ili kufanikisha mabadiliko, tunahitaji
uongozi imara unaoweza kuandaa dira na mikakati inayotekelezeka,
kuanzisha na kusimamia mageuzi na kuwasiliana. Kiongozi asiyeweza
kuongoza mageuzi si kiongozi bora.
“Dunia inabadilika, nchi yetu
inabadilika, matarajio ya wananchi kwa Serikali yanabadilika, hivyo ni
lazima tubadili namna tunavyohudumia wananchi, kwani kuna watu wenye
mitazamo au fikra finyu wanaoshuku madhumuni ya kila mabadiliko,”
alisema.
Balozi Sefue alisema kwa sasa kuna
changamoto za utendaji katika sekta ya umma, ambazo ni udhaifu katika
ukusanyaji wa mapato na kufanya Serikali ishindwe kujigharimia
kikamilifu pamoja na kuwepo malalamiko ya wananchi dhidi ya Serikali.
Alisema changamoto nyingine ni matumizi
ya fedha za umma, ambayo hayaendani na thamani ya fedha na udhaifu
katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: