SERIKALI YAJIBU MAPIGO KWA MTANDAO WA KENYA ULIOANZA KUICHOKONOA TANZANIA


Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene akizungumza  na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam  kuhusu  mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ulioituhumu  Serikali ya Tanzania.
 --------------
Na Fatma Salum-MAELEZO
 
SERIKALI  ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi yake zilizotolewa na mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ujulikanao kama  www.standardmedia.co.ke unaosadikika kuendeshwa na kampuni ya gazeti la The Standard la nchini humo.
 
Akizungumza  na waandishi wa habari leo  jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene , alisema mtandao huo umeripoti kuwa  Serikali ya Tanzania imekataa kuiuzia Kenya gesi asili ya Songosongo jambo ambalo halina ukweli  kwa kuwa  gesi inayozalishwa hivi sasa bado haijafikia kiasi cha kuweza kuuzwa nje ya nchi.
 
Mtandao huo pia umeripoti kuwa Serikali ya Tanzania ilikataa viwanja vyake vya ndege vya kimataifa kutumiwa na ndege zilizopaswa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata wakati wa ajali ya moto iliyotokea kwenye uwanja huo hivi karibuni.
 
Mwambene alifafanua kuwa tuhuma hizo ni za uongo kwani mara baada ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata kuwaka moto, ndege zilizotakiwa kutua uwanjani hapo ziliruhusiwa kutua kwenye viwanja vya ndege vya Tanzania vya Julius Nyerere   International   Airport (JNIA) na Kilimanjaro International Airport (KIA).
 
“Sio kweli hata kidogo kwamba Tanzania ilikataa ndege za Kenya zisitue kwenye viwanja vyake kwa sababu uwanja wa Jomo Kenyata ulipoungua ndege nyingi zilizopaswa kutua katika uwanja ule zilitua kwenye viwanja vyetu na hii pia ilitokana na ukweli kwamba Tanzania na Kenya zinachangia ndege nyingi za nje ya nchi.” Alisema Mwambene.
 
 Aidha Mwambene alikanusha tuhuma nyingine iliyodai kuwa mwaka 2010 Tanzania ilikataa kuiuzia Kenya chakula badala yake ikaiuzia nchi ya Uganda taarifa ambazo si za kweli kwa kuwa mwaka huo nchi nyingi za Afrika zilikumbwa na baa la njaa ikiwemo Tanzania yenyewe. 
 
Hivyo  Tanzania  ililazimika kusitisha utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara kuuza chakula nje ya nchi na hakukuwa na taarifa yoyote ya kuuzwa chakula nchini Uganda.
 
Kutokana na upotoshaji huo Mwambene alisema Serikali ya Tanzania imeutaka mtandao huo kuomba radhi na isipofanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
 
Katika hatua nyingine Mwambene alifafanua kuwa zoezi linaloendelea nchini  la kuwataka wahamiaji haramu wanaoishi hapa kinyume cha utaratibu kuondoka kwa hiari haliwahusu wakimbizi waliopo nchini kisheria. 
 
Pia zoezi hilo linawalenga wahamiaji haramu wote kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Congo DRC, Zambia na Uganda na hakuna serikali ya nchi yoyote kati ya hizo iliyolalamika kuhusu hatua hiyo.
 
“Mpaka sasa zoezi linaenda vizuri hakuna taarifa yoyote ya malalamiko kutoka Zambia, DRC, Burundi, Rwanda wala Uganda na tayari Rwanda imetuma taarifa rasmi kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendesha vema zoezi hilo. 

Kinachoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari ni upotoshaji unaolenga maslahi binafsi.”
 
Akizungumzia usalama wa Watanzania nchini Rwanda, Mwambene alisema hakuna taarifa ya  Mtanzania yeyote kunyanyaswa nchini  humo  na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Tanzania haujakatika.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: