MWANAMKE ANASWA NA SARE ZA JWTZ ...


JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemkamata Saida Mohamed (30), mkazi wa Mwasonga Kigamboni, akiwa na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). 


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 31, mwaka huu, katika eneo la Mwasonga, Kigamboni.

Alisema Saida alikamatwa na suruali saba, mashati saba ya kombati, kofia 10, shati mbili nyepesi, fulana mbili na kofia moja aina ya bareti, vyote vikiwa mali ya JWTZ.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikuwa na begi moja la kuwekea nguo za jeshi, cheo kimoja cha Koplo na mikanda miwili ya kijeshi.

Alisema uchunguzi unaendelea juu ya mwanamke huyo ili kubaini sababu za kumiliki sare za jeshi, kabla ya kufikishwa mahakamani.

Katika tukio jingine, polisi wamemkamata Husein Mkondoa (25), mkazi wa Gongolamboto Mzambarauni, akiwa anaendesha pikipiki huku akiwa amevaa nguo za kiraia na kofia ngumu ya kijani yenye nembo ya Polisi.

Alisema polisi walimtilia mashaka na kumkamata mtuhumiwa na anaendelea kuhojiwa.

“Naomba kutoa onyo kwa watu wote wenye silaha na sare za jeshi wazisalimishe kwa polisi au ofisi yoyote ya Serikali, msako wa kuwakamata wahalifu utakuwa endelevu na tutaingia nyumba hadi nyumba kuwatafuta wahalifu.

“Sambamba na operesheni hii, licha ya kubadilisha uongozi katika kituo cha Polisi Ubungo, tumeamua kutupia macho vitendo vya utapeli katika eneo la Ubungo Bus Terminal, ambalo watu wengi wanajifanya askari.

“Licha ya hilo, tumeunda kikosi cha kutumia video kamera na kamera za picha mnato ili kubaini na kuchukua hatua na nyendo mbalimbali ili kujenga ushahidi wa wahalifu hao wasiepuke mkono wa sheria,” alisema Kova.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kuchonga hati mbalimbali zinazotaka kufanana na za Serikali.

Kamishina Kova, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shadrack Samwel (27) mkazi wa Mbagala Sabasaba na Mwangi Samwel (38) mkazi wa Kimara Baruti.

Alisema watu hao, hawana ofisi maalumu hivyo hufanya shughuli hiyo sehemu yoyote na ofisi zao kuu ni mkoba pamoja na gari ambalo wanatembelea, lenye namba za usajili T 397 ADX aina ya Crester.

“Watuhumiwa hawa, tuliwakuta na mihuri 27 ambayo ni ya Serikali na taasisi binafsi, mihuri ya mawakili wa kujitegemea na wa serikalini, mhuri wa Jeshi pamoja na mhuri wa Serikali za mitaa.

Pia tumewakamata na nakala mbalimbali za SUMATRA, ikiwemo karatasi za kukagulia magari, pleti namba za magari pamoja na nakala mbalimbali za ofisi hiyo,” alisema.

Katika hatua nyingine, polisi wanawashikilia watu watano, akiwamo Enea Dawsoni, ambaye ni mfanyakazi katika Kapuni ya Ndege ya Fast Jet, kwa jaribio la kutaka kupora fedha kiasi cha Sh 60,000,000 katika Kampuni hiyo.

Alisema watuhumiwa hao walinaswa katika Mtaa wa Samora na iligundulika walikuwa wana mawasiliano ya simu.

“Baada ya kuwakamata watu hawa, Polisi walielekea katika ofisi hizo na baada ya kufika walichukua simu ya watuhumiwa hao na kuona ujumbe mfupi wa maneno, ulioeleza kuwa fedha zipo karibu na chooni.

“Polisi walichukua simu ya wahalifu na walipopiga simu hiyo iliyokuwa na mawasiliano na majambazi hao, simu iliita kwa sauti kubwa ndani ya maungo ya mmoja kati ya watumishi wa Fast Jet.

“Mtumishi Enea Dawson alikuwa ameficha simu hiyo sehemu za siri katika nguo zake ambapo aliumbuka na kugundulika kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na majambazi hao,” alisema Kova
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: