JK "NILIKWISHAKABIDHI ORODHA YA WAUZA UNGA"
WAKATI sakata la dawa za kulevya likiwa
limeichafua Tanzania katika uso wa kimataifa, orodha ya majina ya
wanaohusika na biashara hiyo ambayo Rais Jakaya Kikwete alidai kuwa
nayo, amesema amekwishaipeleka kwenye Mamlaka husika.
Rais Kikwete mara
kadhaa amekuwa akisema kuwa anayo orodha ya watu wanaouza dawa za
kulevya hapa nchini, hivyo gazeti hili lilimtafuta kupitia kwa msemaji
wake, kufahamu suala hilo lilikofikia.
Rais Kikwete alisema
orodha ambayo alisema anayo alikwishaikabidhi kwa vyombo husika kwa
ajili ya hatua zaidi.
“Rais atembee nayo mfukoni ya nini?
Hata Nzowa katika taarifa yake alisema
alipatiwa… wamepewa vyombo husika, Serikali haiendeshwi kwa vyombo vya
habari, kuna vingi vinafanyika bila kutangazwa.
Mtafute Nzowa atakwambia
vyema,” alisema Rweyemamu, wakati gazeti hili lilipotaka kufahamu juu
ya orodha hiyo ya Rais ilikofikia.
Orodha ambayo Rais Kikwete amekuwa
akielezwa kuwa anayo, inadaiwa kuwahusisha vigogo mbalimbali nchini,
wakiwemo wabunge, mawaziri na wafanyabiashara wakubwa ambao hata hivyo
imebainika kuwako kwa ugumu wa kuwachukulia hatua, kutokana na kutokuwa
na ushahidi ili kuwabana wahusika.
Kutokana na kauli hiyo ya Rais kupitia
kwa msemaji wake, Gazeti hili liliamua kutafuta moja ya mamlaka
zinazohusika kupambana na dawa za kulevya ili kufahamu juu ya orodha
hiyo iliyokabidhiwa na Rais na hatua ambazo zimechukuliwa.
Mkuu wa
Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Kamishna
Msaidizi (ACP), Godfrey Nzowa, hakukiri wala kukana kupokea orodha hiyo
kutoka Ikulu.
MTANZANIA Jumapili: Kamanda sisi ni MTANZANIA Jumapili,
tumepata taarifa kwamba Ikulu imekupatia majina ya watu wanaojihusisha
na dawa za kulevya, vipi umefikia wapi katika kuishughulikia?
NZOWA:
“Kutoka wapi? Mimi napata kutoka sehemu mbalimbali, tunakuwa na watu
ambao tunakamata na tunawapekua, ikithibitika tunawapeleka mahakamani
Na hivi karibuni nimepatiwa orodha ya watu 261 wanaodaiwa kufanya
biashara hiyo, lakini katika upekuzi wetu hatukukuta kitu.
MTANZANIA Jumapili: Kwa hiyo hao
mliowapekua ndiyo orodha mliyopatiwa kutoka Ikulu?
Nzowa: Siwezi kutaja
moja kwa moja kwa sababu ninapokea orodha kutoka sehemu mbalimbali, kwa
hiyo si salama kutaja jina la mtu.
Siwezi ku ‘mention’ kuwa ni Ikulu
ama nani. Ushahidi wa moja kwa moja haupo, lakini wa kimazingira upo,
tulipeleka kiapo ili washitakiwe Mahakamani. Kwa mujibu wa Nzowa,
wengine zaidi ya 260 waliopatikana na ushahidi wamefunguliwa kesi katika
mahakama za hapa nchini.
Hivi karibuni katika Bunge linaloendelea
Dodoma, kuliibuka hoja ya kuitaka serikali kutaja orodha ya wanaodaiwa
kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alishindwa kufanya
hivyo.
Badala yake, Lukuvi alisema baadhi ya majina ya wabunge
yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara hiyo na
kwamba angetaja majina, Bunge lisingebaki salama.
Lukuvi alisisitiza kuwa serikali haiwezi
kuwataja hadharani kwa haraka, kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa
mahakamani.
Hata hivyo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa
nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya
mwaka 2008 hadi Julai, mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za
kulevya katika nchi mbalimbali za nje.
Pamoja na kukamatwa kwa
Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika
Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam, ambao ni raia wa Iran,
Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.
Sakata la dawa za kulevya nchini
lilitikisa zaidi baada ya kukamatwa kwa wasichana wawili, Agness Gerald
(25) na Mellisa Edward (24) katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo,
Afrika Kusini, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, (JNIA)
wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine kilo 150,
zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 za Tanzania.
Hatua hiyo ilimlazimisha
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwafukuza kazi wafanyakazi
wa JNIA, wanaodaiwa kuhusika na upitishwaji wa mzigo huo, huku baadhi ya
watendaji wakihamishwa vituo vyao vya kazi. Moto huo uliowashwa na
Mwakyembe, ulikuja baada JNIA kutajwa kuwa moja ya chochoro kubwa za
kupitisha dawa hizo, hali ambayo pia imeshuhudia Jeshi la Polisi
kuwaondoa kwa kuwahamisha vituo vya kazi, Kamanda wa Polisi wa Viwanja
vya Ndege, Kamishna Msaidizi (ACP) Deusdedit Kato na Mkuu wa Upelelezi
wa Viwanja hivyo, David Mwafwimbo.
Source:CHADEMA DIASPORA : JK: Nilikwishakabidhi orodha ya ‘wauza unga’
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: