KIGOGO ALIYEFUKUZWA CCM , AFICHUA SIRI NZITO...
HATIMAYE Mwakilishi wa Kiembesamaki,
Mansour Yussuf Himid, aliyevuliwa uanachama na vikao vya juu vya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, ameibuka na kutoa kauli nzito dhidi ya
chama hicho huku akitoa siri ya kutimuliwa kwake.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu
alipotimuliwa katika kongamano la wazi lililofanyika kwenye Ukumbi wa
Bwawani mjini hapa jana, Mansour alisema licha ya kuvuliwa uanachama
hataacha kutetea masilahi ya Zanzibar bila woga.
Waziri huyo wa zamani na aliyekuwa
Mwakilishi wa Kiembesamaki, alifichua siri kuwa alianza kujengewa chuki,
fitina na viongozi wenzake baada ya kuonekana mtetezi na mpigania
masilahi ya Zanzibar, ukiwamo msimamo wake wa kutaka suala la mafuta na
gesi asilia liondoshwe kwenye orodha ya mambo ya muungano.
Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa
katika siasa za Zanzibar, alisema amepokea uamuzi huo kwa moyo mweupe na
hatarajii kwenda mahakamani au kuwania tena uwakilishi wa jimbo hilo
kupitia chama chochote.
“Nimekubali kufukuzwa uanachama na NEC
ya CCM, wenzako kama hawakutaki huna njia ya kujipendekeza kwao,
sitakwenda kortini wala sihitaji kugombea kwa chama chochote cha siasa,”
alisema Mansoor.
Hata hivyo alisisitiza kuwa licha ya
kufukuzwa, ataendelea kutetea masilahi ya Zanzibar bila woga na
hatanyamazishwa kwa vile hiyo ni haki yake kikatiba kama raia huru, pia
kadi yake ya CCM haikuwa kimeo kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Mansoor alisema lengo la Mapinduzi ya
Zanzibar ya mwaka 1964 ilikuwa kutafuta ukombozi na uhuru wa kifikra,
kiuchumi na kidemokrasia na si kufunga au kuzuia mawazo na maoni ya
watu.
Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi katika
siasa za Zanzibar, alisema kuwa alianza kujengewa kinyongo na viongozi
wenzake baada ya kuonekana kuwa ni mtetezi na mpigania masilahi ya
Zanzibar, ukiwamo msimamo wake wa kutaka suala la mafuta na gesi asilia
liondoshwe kwenye orodha ya mambo ya muungano.
“Hapa ndipo nilipoanza kuonekana mnoko,
nikapewa majina mengi na kupigwa. Kwa taarifa yao, sitaacha kupigania
ninachokiamini, nitabaki kuwa mtetezi wa haki na usawa hadi
nitakapokufa, ila sihitaji kuwa mwakilishi wa mahakamani, sina pesa ya
kulipa wanasheria, mshahara wenyewe umekatwa miguu,” alisema Mansoor
huku nyimbo za kimapinduzi zikiimbwa ukumbini.
Alisema kitendo cha CCM kumpima na
kumuona hafai ni haki yao na ataendelea kuheshimu maamuzi hayo, kwa
sababu ndiyo yaliyotolewa na kufikiwa na chama kwa kufuata taratibu
zao.
Alisema malengo yake mengi ya kisiasa
akayaweka wazi ifikapo mwaka 2015 kama ataona kuna haja ya kufanya
hivyo, lakini alisisitiza kuwa hataiacha au kuitupa Zanzibar katika
maisha yake akiwa ndani au nje ya chama chochote.
Akizungumzia muungano, mwanasiasa huyo
alisema yeye ni muumini wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar lakini
alisema kuwa angependa kuona muungano wenye usawa, haki na heshima na si
upande mmoja kuutafuna mwingine.
Kwa upande mwingine alisema kuna baadhi
ya vyama vya siasa vimeanza kumfuata na kumtaka awe mwenyekiti wa taifa
na wengine wakitaka achukue fomu ya kuwania kiti cha Kiembesamaki.
Alilaumu tabia na hulka ya baadhi ya
wanasiasa wa Zanzibar kupenda kubaguana kwa rangi na uzawa na kuongeza
kuwa mambo hayo si mazuri kuyakumbatia kwani hayana mwisho mwema.
Wakati huo huo, Kamati ya Maridhiano Zanzibar imekiri kuwa haina tena uwakilishi wa vyama vya siasa vya CCM na CUF.
Msimamo huo kwa mara ya kwanza umewekwa wazi jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hassan Nassor Moyo.
Moyo alisema kuwa kamati yake ni ya
utetezi na kupigania masilahi ya Zanzibar na kazi yake kubwa ni kudai
hadhi na tunu ya Zanzibar kama nchi na taifa lenye mamlaka na uwakilishi
katika Umoja wa Mataifa.
Msimamo huo umekuja baada ya Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,
kuikana hadharani kamati hiyo na kusema haitambui na wala haina baraka
za CCM wala serikali yake.
Katika kuonesha kuwa kamati hiyo ni ya
wananchi, hata Mratibu wa kongamano hilo ambaye pia ni Mwakilishi wa Mji
Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alipokuwa akimkaribisha Waziri wa Katiba
na Sheria wa SMZ, Aboubakari Khamis Bakari, alisisitiza kuwa anasimama
kuchangia na kutoa maoni yake kama mwananchi na si kwa kofia ya dhamana
yake.
Akizungumza katika kongamano hilo,
Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakari, alisema
rasimu ya mabadiliko ya katiba haifai kwa vile inainyima Zanzibar mambo
mengi ya msingi na kuikandamiza kiuchumi.
Aboubakary alisema muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ni wa mataifa mawili yaliyokuwa na uwakilishi
sawa kama dola, hivyo si haki upande mmoja kuonekana mgeni mwalikwa
katika ushiriki wake.
Aliwataka wananchi kuacha hofu ya kuwapo
kwa muungano wa serikali tatu na kusema jambo hilo halitavunja muungano
au kutokea machafuko.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya
Maridhiano, Eddy Riyami, alitangaza kuhama rasmi CCM na kusema ataamua
baadaye atajiunga na chama gani kama ataona kuna haja ya kufanya hivyo.
Riyami alichukua mjadala mkubwa wakati
wa sakata la kutoweka na kujiuzulu kwa aliyewahi kuwa Mwakilishi wa
Jimbo la Mkunazini, Salum Msabaha Mbarouk, ambaye sasa amehamia CCM.
Source:Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: