RAISI WA RWANDA KAGAME AZIDI KUICHOKONOA TANZANIA..CHADEMA WAJITOSA
*Sasa amgeukia Membe
*Chadema nayo yajitosa
GAZETI la The New Times Rwanda ambalo linatajwa kuwa mshirika wa karibu wa Serikali ya Rais Paul Kagame, nalo limeingia kwenye propaganda za kuwachafua baadhi ya viongozi wa Tanzania.
Baadhi ya vyombo vya habari vya nchi hiyo, vimekuwa vikitumika kumchafua Rais Jakaya Kikwete, ambapo wiki iliyopita gazeti la News of Rwanda liliandika taarifa iliyodai kuwa Rais wa Tanzania amekutana na wapinzani wa Rais Kagame.
Hata hivyo taarifa hiyo ilikanushwa vikali na Serikali ya Tanzania, ambapo iliweka wazi kwamba Rais Kikwete hajawahi kukutana na watu hao waliotajwa na News of Rwanda na kwamba siku zilizotajwa kuwa rais alikutana na watu hao hakuwepo nchini.
Wakati Tanzania ikikemea propaganda hizo chafu, wiki hii gazeti la The New Times Rwanda, limehamishia uchokozi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, kwamba alikutana kwa siri na mmoja wa waasi wa nchi hiyo alipokuwa jijini Washington DC nchini Marekani.
Gazeti hilo katika toleo lake la juzi, liliandika kuwa Membe alikutana na mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Upinzani nchini humo cha Rwanda National Congress (RNC), Dk. Theogene Rudasingwa jijini Washington DC mwishoni mwa mwaka jana.
Habari iliyoandikwa na gazeti hilo, imebainisha kuwa kikao hicho cha Membe na Dk. Rudasingwa kilikuwa na lengo la kumwomba Membe amshawishi Rais Kikwete aonane na waasi hao kwa ajili ya kufanya mazungumzo.
Gazeti hilo lilidai kuwa limepata taarifa hizo kutoka kwenye vyanzo vyake vya habari vilivyokuwapo nchini Marekani mwaka jana, ambapo Membe alikwenda kuhudhuria mkutano ambao haukuwekwa wazi.
Ilielezwa kuwa baada ya Membe kuonana na kiongozi huyo, Januari 23 mwaka huu viongozi wa RNC walifanikiwa kukutana na Rais Kikwete.
Waliotajwa kukutana na Rais Kikwete ni Mratibu wa chama hicho, Dk. Rudasingwa na Mshauri wake, Condo Gervais.
Kabla ya gazeti hili kuandika uzushi huu, gazeti la News of Rwanda lilidai kuwa kundi la waasi la FDLR lilifanikiwa kukutana na Rais Kikwete nchini Tanzania na kwamba waliwakilishwa na Katibu Mtendaji wake, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi ambaye ni kamanda wa operesheni.
Siku chache baadaye, mtandao wa AllAfrika uliandika kwenye ukurasa wake taarifa zilizokuwa zikimkariri, Faustin Twagiramungu akikiri kufika Tanzania na walionana na Rais Kikwete.
Baada ya uzushi huo gazeti dada la hili, MTANZANIA Jumapili lilifanikiwa kufanya mazungumzo na Twagiramungu ambaye ni Rais wa Chama cha RDI-Rwanda (Rwiz Party of Rwanda), ambaye alisema taarifa hizo za AllAfrika ni za uzushi wa hatari uliofinyangwa na makachero wanaofanya kazi kwa maslahi ya Serikali ya Rwanda.
Mbali ya Twagiramungu, pia Dk. Theogene Rudasingwa ambaye alitajwa na News of Rwanda kuwa alikutana na Rais Kikwete, katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu akiwa nchini Afrika Kusini, alipuuza taarifa hizo na kudai kuwa ni mkakati wa Serikali ya Rais Kagame kutaka wapinzani wake wafungwe.
MTANZANIA Jumatano lilifanikiwa kuzungumza na Ofisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbo Ali, ambaye alisema hafahamu kama Membe alikutana na Dk. Rudasingwa.
“Kwakweli sina uhakika na hilo na sifahamu kama kuna siku Membe alikutana na Dk. Rudasingwa,” alisema Mkumbo.
CHADEMA YAJITOSA
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekiah Wenje, ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana wamejitosa kwenye chokochoko hizo za Rwanda kwa kuishauri Serikali ya Tanzania kutafuta jinsi ya kulimaliza suala hilo.
Mbali na ushauri huo pia, Wenje aliishauri Serikali kuhakikisha Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda, Faustin Twagiramungu anaiomba radhi Tanzania.
Wenje amemtaka Twagiramungu aombe radhi baada ya kunukuliwa na mtandao maarufu wa habari za Afrika wa AllAfrika, akisema katika kile kinachoelekezwa kuwa ni mkutano wa ndani uliofanyika katika mji wa Lyon nchini Ufaransa, jinsi alivyosafiri kwa siri kuja Tanzania na kukutana na Rais Kikwete.
Wenje alieleza kushangazwa na kauli za Twagiramungu kukana kukutana na Rais Kikwete, wakati kuna video ambayo inamuonyesha akizungumza nchini Ufaransa akieleza namna alivyosafiri kwa siri kuja Tanzania.
“Tunaiomba Serikali imtake huyu Twagiramungu aombe radhi kutokana na kauli zake, pia apewe barua ya ‘official demand aje open clearly’ na kutueleza ni kwanini anakanusha, wakati kuna video iliyokuwa inamuonyesha akizungumza hayo.
“Pengine watu wa aina ya kina Twagiramungu ndio wanaosababisha migogoro hii kwa maslahi yao binafsi, sasa tunaomba aje akanushe na aombe msamaha,” alisema Wenje.
Aidha Wenje alisema idara ya uhamiaji ni moja ya idara zilizooza hapa nchini, ambapo alihoji kuwa inawezekanaje hao waasi watumie hati ya kusafiria ya Tanzania wakati ni kinyume na mkataba wa Umoja wa Afrika (AU).
Katika kutaka suluhu ya mvutano huo, Wenje alipendekeza Bunge kupitia Kamati yake ya Mambo ya Nje, liunde kikundi kidogo kitakachopewa jukumu la kulizungumzia tatizo hilo na kufikia suluhu, kwani Watanzania wa kawaida hawajui tatizo la mgogoro.
“Sisi Chadema hatutaki kuona nchi jirani ya Rwanda inaingia katika mgogoro na Tanzania, ikumbukwe kuwa vita ni vita hata kama ni kidogo inaweza kuathiri kiuchumi na kijamii. “Tunajua leo ikitokea vita Rais hataumia atalindwa kwa mitutu ya bunduki, lakini atakayekuja kuumia ni Mtanzania wa kawaida, ni vyema tukaimarisha uhusiano wetu na hizi nchi jirani,” alisema Wenje.
0 comments: