ZANZIBAR YATAKA RASIMU YA KATIBA MPYA IWARUHUSU KUJITEGEMEA KWA KILA KITU..!!

http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/1976288/highRes/569881/-/10ih1q9/-/nasoor.jpg

Kamati ya Maridhiano imetoa maoni yake ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutaka Zanzibar ijitegemee karibu kwa kila kitu.

Maeneo inayotaka yaondolewe kwenye Muungano ni uraia na uhamiaji, sarafu na Benki Kuu, mambo ya nje na usajili wa vyama vya siasa.

Kamati hiyo inayounga mkono muundo wa muungano wa Serikali tatu inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassor Moyo, iliwasilisha mapendekezo hayo juzi katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusema kuwa maoni hayo ndiyo mawazo ya Wazanzibari wengi.

Mapendekezo hayo yalisomwa na Mwakilishi wa Mji Mkongwe ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Ismail Jussa katika Kongamano la Katiba lililoandaliwa na kamati hiyo.

Msimamo wa kamati hiyo unaelezwa kuwa chanzo cha mmoja wa wajumbe wake, Mansour Yussuf Himid kuvuliwa uanachama wa CCM, Agosti 26 mwaka huu.

Akisoma mapendekezo hayo, Jussa alisema kwa kuwa Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar uliziunganisha nchi zilizokuwa huru, unatakiwa kuitwa Muungano wa Jamhuri za Tanzania, kusisitiza kuwa rasimu hiyo inatakiwa kueleza wazi kwamba nchi nyingine zinaweza kuingia kwenye muungano huo.

Alisema kamati hiyo imependekeza kuwa mambo ya nje yasiwe suala la muungano na badala yake nchi washirika zisimamie zenyewe eneo hilo.

Alisema kwa kuwa muungano umetokana na nchi mbili  zilizokubali kuungana na kuunda shirikisho,  msingi wa uraia wa shirikisho utokane na msingi wa mtu kuwa raia wa nchi mshirika na si kinyume chake.

“Kila nchi mshirika (Zanzibar na Tanganyika), ibakie na uraia wake na mtu kuwa na uraia wa nchi mshirika ndiko kumpe uhalali wa kuwa raia wa shirikisho,” alisema.

 Pia kamati imependekeza Rais wa muungano ambaye atakuwa na madaraka ya juu katika shirikisho lote kwa mambo yote ya Muungano, hivyo nchi washirika zinapaswa kuwa na haki sawa katika kutoa watu wa kushikilia Baraza la Mawaziri la Muungano, Bunge na Mahakama.

Alisema rasimu inatakiwa itamke wazi kwamba urais wa Muungano utashikwa kwa zamu na kwa kupokezana baina ya nchi washirika yaani Tanganyika na Zanzibar na kwamba Rais atangazwe mshindi baada ya kupata kura zaidi ya asilimia 50 kutoka Tanganyika na Zanzibar.

Alisema badala ya kuendeleza mfumo uliopo sasa wa Makamu wa Rais kupatikana kutokana na mgombea mwenza, marais wa nchi washirika (Zanzibar na Tanganyika) moja kwa moja wawe makamu wa kwanza  na makamu wa pili wa Rais wa Muungano.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: