RAISI WA UGANDA AMKUTANISHA KIKWETE NA KAGAME..
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ameitisha mkutano wa dharura wa
marais wa nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), kujadili hali ya usalama
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa waalikwa
kwenye mkutano huo ambao pia unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Rwanda,
Paul Kagame.
Wakati hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ikidhoofika, katika siku za karibuni, uhusiano wa
Tanzania na Rwanda umekuwa wa shaka hasa baada ya Rais Kikwete kuishauri
Serikali ya Rwanda kukaa na wapinzani ili kumaliza mzozo uliolikumba
eneo la Maziwa Makuu.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo wakati akiwa
katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU),
zilizofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mkutano wa leo utafanyika
kwenye Ukumbi wa Commonwealth Resort, Munyonyo katikati ya Jiji la
Kampala.
Kwa mujibu wa taarifa Rais Museveni ameitisha
mkutano huo hasa kuzungumzia hatua ya Umoja wa Mataifa kupambana na
Kundi la Waasi wa M23.
Mbali na viongozi hao wa Tanzania na Rwanda,
viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo wanatoka Angola,
Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Sudan, na Zambia.
0 comments: