MMILIKI WA MELI ILIYOKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA NCHINI ITALIA NI MBUNGE
USIRI ulikuwa umetawala kuhusu mmiliki
wa meli ya Kitanzania iliyonaswa juzi nchini Italia, ikiwa na tani 30 za
madawa ya kulevya aina ya bangi lakini sasa kila kitu kinaweza kuwekwa
nje bin hadharani kutokana na taarifa mpya.
tunazo ‘data’ kuwa mmoja wa wamiliki wa
meli hiyo ni mfanyabiashara wa Kitanzania mwenye asili ya Bara la Asia
ambaye alipata kuwa memba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika awamu zilizopita.
Jina la mfanyabiashara huyo linabaki
kwenye kapu letu mpaka baadaye tutakapokuwa kwenye mazingira sahihi ya
kumtaja, kwani kufanya hivyo kwa sasa ni kuingilia mamlaka za kisheria
ambazo zipo kwenye uchunguzi makini.
Habari zinafafanua kuwa mbunge huyo,
hamiliki meli hiyo peke yake, bali kuna watu wengine ambao ni raia wa
Visiwa vya Marshall, barani Australia.
Inaelezwa zaidi kwamba watu hao kutoka
Marshall ni mabilionea wakubwa ambao wanamiliki visiwa vitatu kwenye
Bahari ya Pacific ambavyo ni Ujae Atoll, Ujelang Atoll na Lib.
Mabilionea hao ndiyo wenye Kampuni ya
Gold Star Shipping ambayo inajihusisha na utoaji wa huduma za usafiri wa
majini hususan kwa njia ya meli.
Gold Star Shipping ni kampuni
iliyosajiliwa Visiwa vya Marshall lakini kwa ushirikiano na mbunge huyo
wa zamani, waliileta nchini meli yao ya mizigo ya MV Gold Star,
ikasajiliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
MAGUMASHI YALIPOANZA
MV Gold Star ilisajiliwa Zanzibar ili tu
ipate kibali cha kutumia Bendera ya Taifa la Tanzania, kwani baada ya
hapo, imekuwa ikipuyanga kwenye mataifa mengine, ikitoa huduma za
usafiri pasipo kurudi kwenye nchi iliyosajiliwa.
Taarifa za hivi karibuni, zinaonesha
kuwa imeshakwenda na kurudi Misri mara mbili, Algeria mara mbili na
Uturuki, huku Bandari ya Zanzibar ambayo inaitambulisha kama ndiyo
nyumbani kwao, haijapata kutia nanga hata mara moja.
Julai 29, 2013, saa 2:04 asubuhi, ilitia
nanga Bandari ya Said, Misri. Juni 18, 2013, saa 1:05 jioni, iliwasili
Bandari ya Mostaganem, Algeria. Mei 31, 2013, saa 9:04 usiku, ilifika
Bandari ya Iskenderun, Uturuki. Mei 24, 2013, saa 1:04 asubuhi, iliingia
Bandari ya Said, Misri na Aprili 14, 2013, saa 2:02 asubuhi, ilipiga
king’ora Bandari ya Mostaganem, Algeria.
WASIFU WA MELI
Bandari ya nyumbani ni Zanzibar,
imetengenezwa mwaka 1975, watengenezaji ni Kampuni ya Astilleros De
Mallorca, iliyopo Palma De Mallorca, Hispania, mmiliki ni Gold Star
Shipping kutoka Visiwa vya Marshall, meneja ni Gold Star Shipping, ipo
katika jamii ya Hellenic Shipping Register.
WAMILIKI WA ZAMANI
Ilimilikiwa na Ibrahim Junior mpaka
Februari 2011, Breogan I (aliiuza Novemba 2006), Breogan (Machi 2002),
Estela De Mar (Desemba 1996), Inezgane (1996), Puerto Suances (1988) na
Suecia (1985).
NI MADAWA YENYE THAMANI KUBWA
Kwa mujibu wa ripoti za mitandao ya
Waitaliano na Waingereza, MV Gold Star, ilipakia mzigo wa madawa ya
kulevya nchini Uturuki na walikuwa wanafanya jaribio la kuingiza mzigo
huo wenye tani 30 nchini Italia.
Walinzi wa ufukweni kwenye Bahari ya
Mediterranean, waliishtukia meli hiyo na kuizingira, watu waliokuwemo
baada ya kuona hali ni mbaya, waliwasha moto kuiteketeza MV Gold Star
kisha kufanya jaribio la kutaka kutoroka kupitia boti ndogo.
Askari hao wa ufukweni, walishirikiana
na maofisa uhamiaji wa Italia kuwakamata watu tisa ambao walikuwemo
kwenye meli hiyo na baada ya kuwahoji, ilibainika wote wanatokea nchi za
Misri na Syria.
Taarifa kutoka kwa maofisa uhamiaji wa
Italia zinasema kwamba baada ya kuwahoji watuhumiwa, ilibainika waliamua
kuiteketeza meli hiyo kwa moto ili kuondoa ushahidi wa tani 30 za
madawa ya kulevya zilizokuwemo.
Ilibainishwa pia kuwa thamani ya madawa
hayo ya kulevya yaliyokamatwa ni pauni milioni 50 ambazo kwa chenji ya
Tanzania ni shilingi bilioni 126.5.
FEDHA HIZO ZINAWEZA KUENDESHA WIZARA TATU
Kama mzigo huo ungevuka salama na
kuuzwa, fedha hizo zinatosha kuendesha wizara tatu katika Serikali ya
JK, hii ni kwa mujibu wa makadirio na mapato ya matumizi (bajeti), mwaka
wa fedha 2013-2014.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto bajeti yake ni shilingi bilioni 23, Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo shilingi bilioni 30 na Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi
na Mifugo shilingi bilioni 67, jumla shilingi bilioni 120.
Hii inamaanisha kuwa fedha hizo za wauza
unga, zinaweza kuendesha wizara hizo na chenji itabaki shilingi bilioni
6.5 ambazo zinaweza kujenga shule na mabweni mengi tu. Uchambuzi huo ni
kuonesha namna ambavyo wauza unga walivyo watu hatari, kwani wana pesa
nyingi.
ITALIA KAZI WANAYO
Baada ya kuwakamata watuhumiwa hao,
vikosi vya uokoaji nchini humo, kuanzia vya majini, anga na nchi kavu,
viliizingira meli hiyo kuzima moto uliokuwa unaiteketeza.
Mpaka tunakwenda mitamboni, taarifa zilieleza kwamba bado shughuli ya kuzima moto ilikuwa inaendelea.
TANZANIA HAKUNA ANAYEJUA
Tuilifanya jitihada za kuwatafuta watu
mbalimbali wanaohusika na udhibiti wa madawa ya kulevya nchini lakini
hakuna hata mmoja aliyekuwa na taarifa.
Hata Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti na
Kupambana na Madawa ya Kulevya, Godfrey Nzowa, aliliambia akiwa nchini
Ethiopia kuwa hajui chochote kuhusu meli hiyo kukamatwa lakini aliahidi
kufuatilia.
NI SKENDO NZITO KWA NCHI
Kukamatwa kwa meli hiyo kunazidi kuipaka
matope Tanzania, kwani hivi karibuni raia wake wamekuwa wakikamatwa
katika mataifa mengine, wakiwa wanasafirisha madawa ya kulevya.
Vilevile, kuna ile skendo ya meli ya Wairan yenye Bendera ya Tanzania
ambayo iliibua gumzo mwaka huu lakini suluhisho halijapatikana.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: