KANALI ALIYETOROKA JESHINI AIPASUA KICHWA JWTZ ..
LUTENI Kanali Coelestine Seromba
aneyedaiwa kutoroka ndani ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), bado
hajulikani alipo hadi hivi sasa. Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba
ameliambia gazeti hili jana kuwa kazi ya kumtafuta Luteni Kanali Seromba
inaendelea kimyakimya na kusisitiza kuwa suala hilo halihitaji
kutangazia umma wamefikia hatua gani.
Komba alisema wanajeshi kadhaa
walikimbia katika jeshi hilo lakini hawajatangazwa na wao kama jeshi
hawaoni sababu ya kufanya hivyo kwani wana utaratibu wao. “Huyo Luteni
Kanali Coelestine Seromba anayedaiwa kukimbia ni mwanajeshi mtoro kama
wanajeshi wengine watoro na pindi atapopatikana atatiwa hatiani kama
kanuni za jeshi zinavyosema,” alisema Meja Komba.
Akijibu swali aliloulizwa na mwandishi
wa habari hizi kuhusu kuchelewa kukamatwa kwa Luteni Kanali Seromba,
Meja Komba alisema hatua za kumfuatilia si lazima zitangazwe na pia
mahali lilipofikia jeshi hilo katika kumtafuta ni siri yao.
Meja Komba alisisitiza kuwa Luteni
Kanali Seromba hakuondoka na nyaraka yoyote ya jeshi hilo wala vifaa
vyovyote kama inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Komba aliwasihi waandishi wa habari
kuzingatia maadili ya uandishi kwa kuandika habari za kweli na zenye
tija kwa pande zote ili kutojenga chuki baina ya jeshi na taasisi
zingine.
Alitolea mfano kuwa miaka ya hivi
karibuni ambapo baadhi ya wanasiasa walitamka wazi kuwa jeshi hilo
linakula bure hivyo hakuna umuhimu wa kutengewa bajeti kubwa huku
wakisahau jukumu la jeshi hilo ni kulinda amani ya nchi na mipaka yake
ili wananchi waishi kwa usalama.
Meja Komba alitoa mfano wa vurugu
zilizotokea bungeni hivi karibuni kuwa kama Polisi wangeshindwa
kudhibiti vurugu hizo hatua ya mwisho ilikuwa jeshi kuingilia kati,
lakini watu wanadai wanajeshi wanakula bure. “Kikubwa ninachoweza
kueleza hapa ni kalamu za waandishi kutumika vizuri ili kutoweka chuki
kati ya taasisi zingine likiwemo jeshi letu nje ya nchi,” alisema Meja
Komba huku akigusia namna msuguano kati ya viongozi wa Tanzania na
Rwanda ulivyoripotiwa.
“Mengi yaliyoripotiwa ni kama nchi hii
na Rwanda zinaingia vitani na uhasama huo kuhamia kwa wananchi na
kujenga chuki na baadaye kuchukiana na hata kuweza kugombana wenyewe kwa
wenyewe,” alisema.
Pia aliwakumbusha wananchi kuendeleza
amani iliyopo kwani vita vina gharama kubwa na endapo nchi ipo vitani
hata Bunge linaweza kusitishwa kutokana na fedha nyingi kupelekwa katika
mapigano.
Chanzo kimoja kutoka ndani jeshi hilo
kimesema kutoroka kwa Luteni Kanali Seromba aneyedaiwa kukimbilia Rwanda
hakuwezi kuleta tishio lolote ndani ya jeshi hilo.
Pia taarifa zilizopatikana ndani ya
jeshi hilo zinadai kuwa kitengo alichokuwa Luteni Kanali Seromba ni
kitengo cha kawaida na kwamba mafunzo yake hutolewa kimataifa na kila
nchi ina mtu kama huyo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: