JWTZ LAKAMATA WANAJESHI WANNE WA RWANDA WALIOKUWA KONGO WAKIWASAIDIA WAASI WA M23..
ASKARI wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani nchini Kongo (Monusco),
wakiongozwa na vikosi vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wamedai
kuwakamata maofisa wanne wa jeshi la Rwanda, katika mapigano ya wiki
iliyopita nchini Kongo.
Akizungumza na MTANZANIA Jumatano kwa
sharti la kutotajwa jina, mmoja wa askari aliyepo ndani ya kikosi cha
JWTZ huko nchini Kongo, alisema maofisa hao wanashikiliwa kwa mahojiano
zaidi.
Taarifa hizi za sasa zinakuja wakati ambapo kumekuwa na
madai ya muda mrefu, ambayo yamekuwa yakitolewa na Umoja wa Mataifa
pamoja na Marekani kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia waasi wa kundi la
M-23.
Pamoja na kwamba Rwanda imekuwa ikipinga madai hayo, kitendo chake
cha wiki iliyopita cha kuamua kupeleka bataliani mbili zenye wanajeshi
1,700 ili kukabiliana na kile kinachodaiwa kuwa ni kishindo cha vikosi
vya Umoja wa Mataifa vyenye jukumu la kulinda amani katika taifa hilo
lenye utajiri mkubwa kirasilimali, kinatokana na waasi wa M23 kupata
kipigo kikali.
Chanzo chetu hicho kutoka uwanja wa mapambano
nchini Kongo, kililidokeza gazeti hili kuwa maofisa hao wa Jeshi la
Rwanda waliwakamata katika mapigano hayo yaliyodumu kwa zaidi ya wiki
moja, ambayo tayari yamewakimbiza waasi wa M23.
“Askari wa
Rwanda tuliowakamata, ni maofisa wa ngazi za juu kabisa jeshini, tena
walikuwa na sare za jeshi hilo… walikuwa wakiwasaidia hao M23, lakini
kwa kuwa sisi tulikuwa makini tulifanikiwa kuwatandika hadi
tukawakamata,” kilisema chanzo chetu hicho.
Habari za uhakika
kutoka vyanzo vya habari vya kuaminika zinaeleza kwamba, hatua hiyo ya
kuwakamata maofisa hao pamoja na kuondoka kwa waasi wa kikundi cha M23,
imefanikisha kushinda vita hiyo kwa zaidi ya asilimia 95.
Mtoa
taarifa wetu huyo kutoka Kongo, ameliambia gazeti hili kuwa, tayari
Monusco wanaoongozwa na JWTZ wameanza kufurahia ushindi huo na kwamba
sasa hivi wanasubiri tamko kutoka kwa wakuu wao, ili kufahamu
kinachofuata baada ya kufanikisha hatua hiyo.
MAPIGANO YALIVYOKUWA
Akielezea namna walivyofanikiwa kutoa
kibano kwa M23, askari huyo kwanza alikiri kuwa mapigano yalikuwa
makali, kutokana na kikundi hicho cha waasi kusheheni vifaa vya kisasa
na msaada wanaoupata kutoka Serikali ya Rwanda.
“Kwa kweli
mapigano yalikuwa makali sana, lakini kwa upande wetu sisi tulikuwa
tunajiamini kutokana na vifaa ambavyo pia ni vya kisasa hususani
ikizingatiwa jeshi letu ni la Umoja wa Mataifa.
“Tulifanikiwa kuteka ngome yao kwa kutumia mbinu mbalimbali za kijeshi na kuwafanya watawanyike kabisa katika eneo hilo.
“Ngome
yao ilikuwa ni kubwa sana, ina ukubwa wa zaidi ya viwanja vitatu vya
mpira… na katika eneo hilo kulikuwa kumesheheni vifaa vyao vya kivita,
kama makombora, mafuta, mizinga pamoja na vifaa vingine kama magari na
baadhi ya silaha nyingine kubwa kubwa za kivita,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, sasa hali ni shwari ndani ya nchi hiyo ya Kongo.
“Baada
ya kuwasambaratisha sasa wamekimbilia eneo moja lililopo karibu na
mpaka wa Uganda. Kama unavyofahamu hawa jamaa walikuwa wakitumia mbinu
za kujihami kwa kurusha mabomu katika eneo la Rwanda, ili ionekane kuwa
sisi tumerusha,” alisema askari huyo.
“Lakini tunamshukuru Mungu,
tupo salama ingawa tumempoteza askari mmoja na askari wengine wenzetu
wa Tanzania ambao ni wanne, wamepata majeraha kidogo lakini wanaendelea
vizuri.
“Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu waendelee kutuombea
turudi salama, kwa sababu kazi sasa imeshakamilika,” alisema askari
huyo.
Juhudi za gazeti hili kumpata msemaji wa Monusco, Luteni Kanali Prosper Basse kuzungumzia juu ya taarifa hizo, zilishindikana.
Taarifa
ambazo tumezinasa kwa siku kadhaa sasa kutoka uwanja wa mapambano na
ambazo zimegusa vichwa kadhaa vya habari zinaeleza kuwa, brigedia
maalumu ya vikosi vya UN yenye dhamana ya kujibu mashambulizi (FIB),
katikati ya wiki iliyopita iliendesha operesheni kubwa iliyoharibu
kabisa ngome muhimu ya waasi wa M23, hali inayotajwa na wachambuzi wa
mambo kuwa ndiyo iliyoishtua Serikali ya Rwanda ambayo inatuhumiwa
kuwasaidia waasi hao.
Taarifa za kijeshi zinaeleza kuwa, FIB
ambayo inaundwa na wanajeshi wapatao 3,000 kutoka Tanzania na Afrika
Kusini chini ya Azimio Namba 2098 la Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa, limejizatiti kwa zana za kisasa za kivita zikiwamo mizinga na
helikopta za kivita.
Taarifa kutoka mashariki ya Kongo zinaeleza
kwamba, mashambulizi dhidi ya waasi wa M23 ambao hivi karibuni
waliripotiwa kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Tanzania aliye
katika jeshi la UN, yamesababisha waasi hao kukimbilia katika eneo la
milima lililopo umbali wa kilomita tano kutoka mji mdogo wa
Kanyaruchinya Mashariki mwa Goma.
M23 WAZUNGUMZA
MTANZANIA Jumatano jana lilifanikiwa
kuzungumza na Rais wa M23, Bertrand Bisiimwa, ambapo pamoja na mambo
mengine alieleza sababu za vikosi vyao kuondoka katika ngome yao ya
kivita sambamba na taarifa za kuibuka kwa mapigano mapya ya hivi
karibuni.
Katika hilo, Bisiimwa alikiri kikosi chake kurudi nyuma
siku nne zilizopita, huku akiitaja sababu ya kufanya hivyo kuwa
ilitokana na wao kutotaka vita baada ya majeshi ya Kongo kuanza
kuwarushia mabomu kwenye kambi yao.
“Sisi tuliamua kurudi nyuma
tusiendeshe vita, tunajua aliyetupa hayo mabomu ambayo yalifika mpaka
Rwanda, tunaitaka Umoja ya Mataifa ikuje ifanye uchunguzi wake…wakuje
waangalie vifaa yetu waone kama inaweza kurusha mabomu hadi Rwanda,”
alisema.
Hata hivyo, Bisiimwa alisema kuwa sio kweli kama majeshi
ya Umoja wa Mataifa yakiongozwa na JWTZ yaliwasambaratisha katika ngome
yao.
“Sio kweli walikuja Kanyaruchina tukiwa tumeondoka na
tuliondoka si kwa sababu ya kuwakimbia, hapana tulitaka UN wafanye
uchunguzi yake juu ya kurushwa mabomu, kwa sababu wanataka kutuvalisha
mambo ya uongo mchafu,” alisema Bisiimwa.
Bisiimwa alijigamba
kuwa majeshi ya Kongo hayawawezi na kwamba walikwishawashindwa, lakini
akakiri kwamba majeshi ya Umoja wa Mataifa wanaweza kuwaondoa.
“Ninakiri
hiyo kwa sababu Umoja wa Mataifa inaweza kututoa, unajua inakuwa na
nguvu ya hatari,” alisema Bisiimwa kwa Kiswahili cha tabu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: