MVUTANO MKALI WA KISHERIA, KESI YA VIGOGO WA UNGA.

Mvutano mkali wa kisheria uliibuka jana Mahakama Kuu baada ya upande wa mashtaka kutaka kuongeza shahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi ya dawa za kulevya inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina la Mama Leila na wenzake saba.
 
Ubishi mkali ulianza pale Wakili Mwandamizi wa Serikali, Prosper Mwangamila alipowasilisha ombi la kuongeza shahidi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Eva Mamuya ambaye alizifanyia dawa hizo uchunguzi wa kimaabara.

Mbele ya Jaji Grace Mwakipesile anayesikiliza kesi hiyo, Mwangamila alisema: “Kwa vile kesi hii inahusu dawa za kulevya, tunaomba shahidi huyu aweze kupata nafasi ya kutoa ushahidi wake”.

Mwangamila ambaye anasaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Maugo aliongeza kuwa mashahidi wote watakaofika mahakamani watatoa ushahidi unaohusu dawa alizofunga Mamuya, hivyo lazima awepo mahakamni kwa ajili ya kuzifungua.

Kwa kuzingatia mazingira hayo, wakili huyo aliiomba Mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo hadi leo, ili waweze kuwasilisha taarifa ya kumwongeza shahidi huyo katika mashahidi wao, kwa mujibu wa kifungu cha 289 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hoja hiyo ilisababisha mabishano ya kisheria pale mawakili wa utetezi wakiongozwa na Yassin Membar walipopinga ombi kwa maelezo kwamba kifungu hicho kinautaka upande wa mashtaka kutoa sababu za kuridhisha za kutaka kumwongeza shahidi mpya, baada ya usikilizwaji wa awali wa kesi katika Mahakama za chini.

Usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo ulifanywa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Mawakili hao pia waliutaka upande wa mashtaka kuendelea na ushahidi wa shahidi mwingine waliyekuwa wamemwandaa.

Wakili mwingine wa utetezi, John Mapinduzi aliomba Mahakama itupilie mbali ombi la Jamhuri, akidai kuwa linalenga kuwahujumu wateja wao na kwamba ushahidi huo haukuwapo awali, badala yake unataka kupikwa.

Jaji Mwakipesile baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hilo hadi leo kwa ajili ya kutoa uamuzi wa ombi hilo la upande wa Jamhuri.

Mama Leila ambaye pia hujulikana kwa majina ya Naima Mohammed Nyakiniwa, anadaiwa kuwa mfanyabiashara wa dawa za kulevya wa kimataifa ambaye amewahi pia kutajwa na Rais wa Marekani, Barrack Obama, kuwa ni mtu hatari kwa biashara hiyo.

Katika kesi hiyo yeye na wenzake wanakabiliwa na shtaka la kuingiza nchini Tanzania dawa za kulevya aina ya Cocaine, zenye uzito wa kilo 5 ambazo zinadaiwa kuwa na thamani ya Sh225 milioni.

Washtakiwa wengine Antony Arthur Karanja na Ben Ngare Macharia (wote Wakenya); na Watanzania watano; Sarah Munuo, Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Juma Mzome na John William.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 3, 2011, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na kusomewa shtaka la kuingiza nchini dawa hizo, wakidaiwa kukiuka kifungu cha 16 (1) b (i) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009.

Walikamatwa na Polisi Juni Mosi, 2011, eneo la Mbezi Beach, katika nyumba inayomilikiwa na Mama Leila, wakiwa na dawa hizo.

Awali kesi hiyo ilikuwa imepangwa kusikilizwa katika Ukumbi Namba Tatu wa Mahakama, ambao ulikuwa umefurika kutokana na kuchanganywa washtakiwa wa kesi tatu tofauti, lakini baadaye washtakiwa walilazimika kuhamishiwa Ukumbi Namba Moja wa Mahakama hiyo.

Wakati wakiingizwa katika ukumbi huo, washtakiwa hao, hususan wanawake walikuwa wakificha nyuso zao kwa kujifunika kwa mitandio waliyokuwa wamejitanda vichwani ili kuwakwepa wapiga picha.

Baada ya Jaji Mwakipesile kuingia mahakamani na watuhumiwa kutambulishwa, alibaini kwamba walikuwa wamekaa shaghalabagala, hivyo aliwaamuru wakae kwa kufuata mpangilio, akianza mshtakiwa wa kwanza hadi wa mwisho.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: