DHAMANA YA SHEKHE PONDA KUJULIKANA LEO..


Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, leo inatarajiwa kuamua iwapo Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, anastahili dhamana au la, kutokana na kesi inayomkabili.

Shekhe Ponda alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 na kusomewa mashitaka matatu ya uchochezi yanayomkabili.

Upande wa mashitaka ulidai mahakamani hapo kuwa utaleta mashahidi 15 na vielelezo vitatu, ili kuthibitisha mashitaka hayo.

Baadhi ya vielelezo vitakavyotolewa mahakamani hapo ni pamoja na DVD mbili, kibali kilichotolewa Agosti mosi cha kongamano la Kiislamu, kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro (OCD) na Hati ya Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kesi hiyo ya jinai namba 128 ya mwaka 2013, iko mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Morogoro, Richard Kabate.

Shekhe Ponda katika kesi hiyo, anatetewa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Juma Nasoro, wakati upande wa mashitaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola.

Shekhe Ponda anadaiwa kutenda kosa la uchochezi Agosti 10 saa 11:45 jioni katika eneo la Kiwanja cha Ndege mjini Morogoro.

Inadaiwa siku hiyo Ponda alialikwa kutoa maelezo machache katika kongamano la Idd lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Mkoa wa Morogoro (Uwamo), na akiwa hapo alitoa maneno ya uchochezi.

Shekhe Ponda anadaiwa kusema: “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza la Waislamu Tanzania), ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao, na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana.

Wakili Kongola alidai kuwa kwa kufanya hivyo, Shekhe Ponda alivunja masharti ya hukumu ya kifungo cha nje iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, iliyomtaka kuhubiri amani.

Katika madai ya pili Shekhe Ponda anadaiwa kushawishi Waislamu kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia:“ Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuua, kubaka na kutesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.

“Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliokataa Mwarabu kupewa kipande cha ardhi ya uwindaji, baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.”
 
Baada ya kusomewa maelezo hayo ya tuhuma zinazomkabili, Shekhe Ponda alikana mashitaka yote huku akikubali kuwemo kwenye kongamano hilo, kukamatwa na Polisi Agosti 11 Dar es Salaam na jina lake kuwa sahihi kama lilivyoandikwa katika hati ya mashitaka.

Wakili anayemtetea Shekhe Ponda aliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja wake, kwa madai kuwa mashitaka hayo yote kisheria yana dhamana.

Hata hivyo Wakili Kongola, aliiomba Mahakama kumnyima dhamana kwa madai kuwa ombi hilo halina msingi wowote na kutokana na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP), kupinga dhamana ya mshitakiwa kwa maslahi ya usalama wa nchi.

Akitoa mwongozo wa maombi yaliyowasilishwa na pande zote mbili, Hakimu Kabate alisema hawezi kutoa uamuzi kwa kuwa kesi hiyo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kuamua kuiahirisha na kupanga Septemba 11 ambapo kesi hiyo ilitajwa.

Hata hivyo, alisema leo Mahakama itatoa uamuzi endapo mshitakiwa atapewa dhamana au sivyo na kesi hiyo itaanza kusikilizwa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: