KISUMO "CCM INAWEZA KUNG'OKA MADARAKANI KWA JINSI INAVYONYAMAZIA UFISADI


Mwanasiasa na kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo ameonya kuwa chama hicho kinaweza kuondolewa madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.

Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika mazungumzo maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake Dar es Salaam kuhusu kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere inayoadhimishwa leo.

Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba kimemeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku kikishindwa kuidhibiti rushwa na kuwajibisha wahusika wa vitendo hivyo.

“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:

“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini. Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere haukuwapo.”

Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.

Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.

Alitoa mfano wa tuhuma za baadhi ya viongozi wa Serikali kuficha mabilioni ya shilingi kwenye benki za Uswisi, kuwa zinaweza kuwa kete muhimu ya kuwaingiza Chadema madarakani, iwapo Serikali ya sasa haitawashughulikia wahusika.

“Wakijitokeza na kuwataja majina wahusika, wakasema fulani na fulani ndiyo wenye mabilioni haya Uswisi, na Serikali ikasita kuwachukilia hatua, wakasema tukiingia madarakani tutawakamata, wananchi wanaweza kuwaamini na kuwachagua,” alisema na kuongeza: “Wakishinda uchaguzi hata kwa viti vichache tu, watakosa nguvu bungeni, lakini kwa wananchi watakuwa na nguvu sana.

Hii inaweza kuwasaidia kwa miaka mitano ya kwanza. Wanaweza kupata ushindi mkubwa zaidi kwa mara ya pili na wakiingia madarakani watawafunga viongozi wa zamani kweli.”

Mzee Kisumo anasistiza, “Hili linawezekana. Anayesema uwezekano wa CCM kushindwa haupo, anajikana mwenyewe. CCM inabidi ijihami na majibu ya jinsi inavyotumia rasilimali za nchi.”


Alionya kuwa si vizuri kuishia kujinadi kwa mambo mengi mazuri iliyofanya huko nyuma, akitolea mfano kuwa hiyo ni sawa na nguo nyeupe ambao ikiingia doa moja tu inakuwa haitamaniki tena.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: