WAPINZANI WAMPONDA RAIS KIKWETE., WADAI AKIENDELEZA KEJELI DAMU ITAMWAGIKA.

SIKU moja, baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema anashangazwa na uongo wa baadhi ya wanasiasa kumtuhumu juu ya mambo mbalimbali kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, viongozi wa vyama vitatu vya upinzani wameibuka na kusema madai hayo hayana msingi wowote.

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi).

Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya kumalizika kikao kati yao na viongozi wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, walisema endapo Rais Kikwete atasaini muswada huo kwa kutegemea nguvu ya dola, ataingiza nchi kwenye machafuko.

Kwa upande wake Mbowe, alisema kama Rais atachukuliwa mzaha na kuamua kusaini muswada huo bila kufikiria maslahi mapana ya taifa, nchi itaingia kwenye machafuko na kamwe nguvu ya dola haiwezi kushinda nguvu ya umma.

“Tunarudia kumshauri na kumsihi Rais Kikwete, Katiba ni haki ya Watanzania wote inahitaji busara, ushirikiano, uvumilivu, staa, kuangalia maslahi, kuaminiana na vitu vingine kama hivyo.

“Kama atapuuza na kuanza kukejeli malalamiko yanayotolewa na makundi mbalimbali na kuamua kusaini, hakika taifa litaingia kwenye machafuko, hawezi kupuuza Shura ya Maimamu yenye Waislamu wengi na makundi mengine.

“Kamwe hatuwezi kupiga magoti kwa kuomba Katiba Mpya, hii si zawadi kwa wanasiasa na hatupiganii kupatikana kwa Katiba nzuri kwa maslahi yetu wenyewe, bali kwa Watanzania wote, ndio maana nasema hatuwezi kuomba, tunataka Katiba Mpya iliyoshirikishwa makundi yote.

“Katika suala hili, kuna uwezekano wa kutokea shari au heri, lakini kwa upande wetu hatupo kabisa kwenye shari bali tunataka pawepo na heri kwa kufungua milango, ili kila kundi lisikilizwe na lipate uwakilishi sehemu pale panapowezekana,” alisema.

Kwa upande wake, Profesa Lipumba alisema Rais Kikwete ameanza kuonyesha mwenendo ambao si mzuri kwa maslahi ya taifa.

“Kwanza naomba niseme, Rais Kikwete kawadanganya Watanzania huko Califonia nchini Marekani kupitia jumuiya yao, kule amekwenda kupumzika, asitumie nafasi hiyo kuficha ukweli.

“Tunasema yeye anadanganya, kuliko baadhi ya wanasiasa hao anaowasema, tunataka atambue Katiba ni ya Watanzania wote na sio ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),” alisema.

Naye, James Mbatia wa NCCR Mageuzi, alisema kama Rais Kikwete anadai ametumia mapendekezo ya wadau kuteua wajumbe, anapaswa kumweka wazi anayewakilisha kundi la walemavu.

Alisema Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), lilipendekeza majina matatu ili achaguliwe mmojawapo, lakini wote walitupwa nje na kulifanya kundi hilo kujiona halina umuhimu ndani ya jamii.

“Kama kweli anajua ameongozwa na mapendekezo hayo, asimame atueleze kila kundi limewakilishwa na nani, yapo mambo mengi tunayolalamikia tunataka haki itendeke kwa kila Mtanzania,” alisema.

Kwa upande wake, Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Mussa Yusuph Kundecha, alisema wameungana na upinzani kudai Katiba iliyokidhi matakwa ya Watanzania.

“Tumejadiliana na kuafikiana kuungana, ili Katiba ipatikane yenye mawazo ya makundi yote, kwa bahati nzuri malalamiko yetu Waislamu yamekuwa na uwiano sawa na malalamiko ya wapinzani.

“Sasa kama wote tumekutana na wazo au shida moja, lazima tuamue tufanye nini ili tupate jibu, sasa tunataka muswada urudi bungeni ujadiliwe upya ili kuondoa upungufu uliopo na vipengele vilivyochomekwa kinyemela.

Juzi Rais Kikwete akiwa Marekani alisema anasikitishwa na baadhi ya wanasiasa kueneza uongo kwa kudai hakufuata mapendekezo ya wadau katika kuteua wajumbe, jambo ambalo analipinga.

-Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: