DAKTARI FEKI ANASWA KATIKA HOSIPTAL YA MUHIMBILI JIJINI DAR ES SALAAM..

DAKTARI anayedaiwa kuwa bandia amekamatwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, akiwa na vitambulisho bandia vya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) akisomea Shahada ya Pili.
 
‘Daktari’ huyo ambaye amekuwa akitafutwa na uongozi wa chuo kwa zaidi ya mwaka alikamatwa jana asubuhi akiwa hospitalini hapo karibu na jengo kilimo kitengo cha meno.
Katika kitambulisho chake cha kupigia kura anatambulishwa kwa jina la Dismas John Macha aliyezaliwa mwaka 1979 Kilimanjaro na anaishi maeneo ya Upanga Magharibi, Dar es Salaam.
 
Gazeti hili, lilimshuhudia mtuhumiwa huyo akiwa katika kituo cha usalama cha Muhas na kupekuliwa na askari Polisi wa Muhimbili, Anthony Mwamatepela na kukutwa akiwa na vifaa vya udaktari .
 
Baadhi ya vifaa alivyokutwa navyo ni pamoja na koti jeupe la udaktari na stetoskopu ambacho ni kifaa cha kusikilizia mapafu yanavyofanya kazi na mapigo ya moyo.
 
Pia alikuwa na begi jeusi lenye aina mbalimbali za dawa, vitambulisho na karatasi nyingi, lakini alipoulizwa alidai kuwa hizo ni dawa zake.
 
Macha alikutwa pia na vitambulisho vitatu tofauti, kimoja kikimtambulisha kuwa mwanafunzi wa Muhas wa Shahada ya Pili ya Udaktari (Masters of Medicine ) yenye jina la Macha Dismas kikionesha kusajiliwa kwa namba 60520/2011 na kumaliza muda wake Septemba 30 mwakani. Kitambulisho kingine kilimtambulisha kwa jina la Macha Rogers anayesoma Shahada hiyo hiyo ikionesha kuwa anamaliza masomo yake mwakani.
 
Alikutwa pia na kitambulisho kinachomwonesha kuwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza na kadi ya anuani yenye jina la Amos Nnko ambaye ni Ofisa Rasilimaliwatu wa Chuo hicho.
 
Akizungumzia alivyomkamata askari wa chuo hicho, Fulgence Semfukwe alisema walimkamata baada ya kupata taarifa za yeye kuwa maeneo hayo na kupanga mbinu za kumkamata.
Saa 4.45 asubuhi jana alimkuta kwenye jengo la meno na kumwomba kwa nafasi yake ya udaktari amsaidie tatizo lake na hivyo waongee pembeni, naye bila wasiwasi akakubali. Alimwuliza anatibu magonjwa gani naye kumjibu anatibu maradhi ya aina nyingi na kumwomba kitambulisho na yeye kumpa cha kwake.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: