ASKOFU KULOLA AMETESEKA SIKU 365 ....
Marehemu
Kulola aliyefariki dunia saa 5:35 juzi baada ya kusumbuliwa na matatizo
ya moyo na mapafu, alianza kusumbuliwa na maradhi hayo karibu mwaka
mmoja uliopita.
KILA mtu anajua kufariki dunia kwa aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la
Evangelist Assemblies of God (EAGT), Moses Kulola katika Hospitali ya
African Medical Investment (Ami) iliyopo wilayani Kinondoni jijini Dar.
ASKOFU KULOLA AMETESEKA SIKU 365
Kwa mujibu wa mjukuu wa marehemu, Flora Mbasha, baada ya hali yake
kutoridhisha, alipelekwa nchini India kwa matibabu zaidi lakini hata
aliporudi hali yake haikuwa nzuri.
FLORA MBASHA AZIMIA
Hata hivyo, baada ya kuzungumza na Flora alipata mshtuko wa kifo hicho cha babu yake.
Alipelekwa hospitali na mumewe, Emmanuel Mbasha na ndugu wengine ambako
alipumzishwa kwa karibu nusu saa. Mbasha alilihakikishia gazeti hili
kuwa kweli mkewe alipoteza fahamu na kutokana na msiba huo, amelazimika
kuahirisha shoo kubwa ambayo ilikuwa ifanyike Septemba 15, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ndugu wengine, marehemu Kulola ameishi duniani kwa miaka
85, alizaliwa 1928, Mwanza katika familia yenye watoto kumi, watano
wakiwa wameshatangulia mbele ya haki.
WATOTO KUMI
Marehemu alifunga ndoa na Elizabeth Kulola na kujaliwa kupata watoto kumi, watatu wakiwa wametangulia mbele ya haki.
Uhakika wa idadi ya wajukuu aliowaacha hauko wazi, lakini habari
zinasema ameacha wajukuu zaidi ya 45 na vitukuu kibao kwa mkewe
Elizabeth.
AANZA KUHUBIRI
Mwaka 1962
alianza kuhubiri akiwa mfanyakazi wa serikali. Mwaka 1964 ndipo
alipoamua kuweka nguvu zake zote katika kumtumikia Mungu huku akiwa
anasomea utumishi wa Bwana. Mwaka 1966 alimaliza masomo akiwa na
stashahada.
AANZISHA MAKANISA ELFU NNE
Mwaka 1992 ndipo alipoanzisha kanisa la EAGT ambalo lilipata mafanikio
makubwa sana katika nchi za Tanzania, Malawi na Zambia na yeye kuwa
askofu mkuu akiwa na msaidizi wake, Mwaisabira wakisimamia makanisa elfu
nne katika maeneo hayo.
WACHUNGAJI WALIOTOKANA NA YEYE
Marehemu atakumbukwa kwa kuzalisha watumshi wengi wa Mungu nchini
Tanzania wakiwemo, Dr. Daniel Moses Kulola (mwanaye), Mchungaji Florian
Katunzi, Askofu Zakaria Kakobe, Antony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’,
Dunstan Maboya, Mwasota na wengineo wengi.
ALIAMURU NYWELE ZAKE ZISIREFUKE
Katika utumishi wake inadaiwa marehemu hajawahi kwenda saluni kupunguza
nywele kwa miaka 47 iliyopita baada ya kuziamuru kwa jina la Yesu
zisirefuke.
Mpaka tunakwenda mitamboni, msiba wa marehemu Moses
Kulola ulikuwa Kanisa la EAGT Temeke, Dar. Mwili wa marehemu
umehifadhiwa Mission Mikocheni Hospital ‘Kwa Kairuki’ kabla ya
kusafirishwa Mwanza kwa mazishi.
Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amin
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: