
HUWEZI kuacha kutafsiri kwamba, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda anawahenyesha askari wa Dar es
Salaam tena kwa saa 24, Ijumaa Wikienda limegundua.
Hali hiyo imesababishwa na ulinzi mkali anaotakiwa kupewa Shehe Ponda
na askari wa jela kwenye Magereza ya Segerea, Dar baada ya kupokea
mzigo huo wa kumlinda kutoka kwa askari polisi na usalama wa taifa
alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili.
Wiki mbili zilizopita akiwa kwenye mhadhara mjini Morogoro, Shehe Ponda alidai kupigwa risasi kwenye bega la kulia.
Wakati wa tukio hilo, Ponda alikuwa akisakwa na polisi kwa kosa la
kutoa hotuba yenye uchochezi akiwa Zanzibar huku akijua yupo ndani ya
kifungo cha nje cha mwaka mmoja ambacho kinataka asipatikane na shitaka.
Akizungumza na gazeti hili juzi jijini Dar, afande mmoja kutoka jeshi
la polisi (aliomba hifadhi ya jina) alisema polisi wanamshukuru Mungu
Ponda kupelekwa Seregea, wenzao wa magereza nao wakahenyeshwe na ulinzi.
“Unajua nini ndugu mwandishi? Kumlinda Ponda ni kufa na kupona,
popote unapokuwa naye awepo, wenzake wanaweza kuvamia na kuvunja amani, wewe
una bunduki wao hawana silaha, unafanyaje hapo?” alisema afande huyo.
Uchunguzi zaidi wa Ijumaa Wikienda umebaini kuwa, baadhi ya askari
polisi walikuwa wakikwepa kushika zamu ya kumlinda Ponda Muhimbili kwa
kuona ugumu wa kudhibiti vurugu endapo wafuasi wake wangeamua
kukinukisha.
Mei 9, mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
ilimhukumu Ponda kifungo cha nje cha mwaka mmoja jela. Ponda na wafuasi
wake 49 (waliachiwa huru) walidaiwa kakaidi agizo la jeshi polisi kwa
kufanya maandamano haramu Februari 15, mwaka huu kwenda katika ofisi za
DPP.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: