WANAFUNZI WAPIGA KURA ZA SIRI ILI KUWAFICHUA WALIMU WANAOFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI


KATIKA hali isiyo ya kawaida, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyasubi, iliyopo Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, wamepiga kura za siri ili kuwafichua walimu wenye tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi wao shuleni hapo.

Uamuzi wa kupigwa kura hizo ulifikiwa hivi karibuni kwenye Kikao cha Baraza la Shule la Watoto ambacho kiliitishwa kwa lengo la kujadili vurugu zilizokuwa zikijitokeza shuleni hapo na kusababisha baadhi ya walimu kupigwa.

Kikao hicho kiliitishwa na Mratibu wa Mradi wa Haki Yangu Sauti Yangu, mkoani humo, Bw. Gerald Ng’ong’a na
Kkubaini kuwa, sababu moja wapo iliyochangia vurugu hizo ni baadhi ya walimu kufanya mapenzi na wanafunzi wao.


Inadaiwa hali hiyo pia imechangia wanafunzi wengi waliomaliza kidato cha nne shuleni hapo kupata matokeo mabaya, kuporomoka kwa kiwango cha elimu kutokana na walimu kutotimiza wajibu wao kikamilifu.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza katika kikao hicho, walisema chanzo cha vurugu ni wanafunzi wa kiume kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi wa kike hivyo wanachukizwa na kitendo cha baadhi ya walimu kutembea na wapenzi wao.

Walisema kutokana na hali hiyo, wanafunzi wa kiume waendapo mitaani hujiunga na vikundi vya wahuni ambao huchukua hatua za kuwateka na kuwapiga walimu wao ili kulipa visasi.

Hata hivyo, wanafunzi hao walipotakiwa kuwataja walimu wenye tabia hiyo waliomba ufanyike mchakato wa upigaji kura za siri ambapo kazi hiyo ilisimamiwa na walimu pamoja na wazazi walezi ambao walishiriki kikao hicho.

Kura hizo ziliwataja majina ya baadhi ya walimu wenye tabia hiyo na majina ya wanafunzi wanaoshiriki kufanya nao mapenzi lakini hazikutangazwa kwa kuwa ni siri na zitawasilishwa kwa uongozi wa shule ili wahusika waitwe na kuonywa.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wanafunzi shuleni hapo walilalamikia kitendo cha walimu wao kuwapa adhabu kubwa zisizolingana na makosa wanayoyafanya wakitolea mfano wa adhabu ya kugaragazwa chini kwa kosa la kutokutoa ada ambalo walisema si kosa lao bali ni la wazazi.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Ng’ong’a, aliwashauri wazazi, walezi kuhakikisha wanafanya vikao vya mara kwa mara ili waweze kurejesha hali ya amani na utulivu shuleni hapo.

"Nimesikitishwa kusikia miaka minne hamjaitisha kikao chochote cha Bodi ya Shule wala cha wazazi, hali hii inachangia mambo mengi kutopatiwa ufumbuzi wa haraka pale yanapojitokeza.

"Ni muhimu kuwa na vikao vya mara kwa mara pamoja na Baraza la Shule la Watoto ili kutoa fursa ya kusikiliza kero mbalimbali walizonazo," alisema Bw. Ng’ong’a.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: