ZAOHAKUNA
lugha nyingine zaidi ya kusema Zenji (Zanzibar) sasa hapakaliki hasa
kwa viongozi wa dini, achilia mbali raia wa kigeni kufuatia kushamiri
kwa vitendo vya kuwadhuru kwa tindikali au silaha, Ijumaa Wikienda lina
mfululizo wa mikasa na ifuatayo ndiyo ripoti kamili.
Padri Joseph Onesmo Mwang’amba akiwa hospitalini baada ya kumwagiwa tindikali.
Ukiachilia mbali mnyororo wa matukio hayo yaliyosababisha makovu,
ulemavu na vifo, tukio ambalo halijapoa ni la Ijumaa iliyopita ambapo
Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui, Zanzibar, Joseph Onesmo
Mwang’amba (60) kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.
Tukio hilo
lenye kuunga na mengine nyuma, lilijiri nje ya duka la huduma ya
mawasiliano ya intaneti la Shine Shine lililopo Mtaa wa Mlandege Mkoa wa
Mjini Magharibi, Zanzibar ambako padri huyo alikwenda kuperuzi.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Afande Haji Hana alikiri
kutokea kwa tukio hilo ambalo lilimfikisha mtumishi huyo wa kiroho
kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja ambako anaendelea na matibabu.
Shehe Fadhil Suleiman Soraga baada ya kumwagiwa tindikali.
Tindikali hiyo ilimjeruhi padri sehemu za usoni, kifuani na mkono wa kulia.
Novemba
6, 2012; Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shehe Fadhil Suleiman Soraga
alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana. Alijeruhiwa usoni na
mwilini.
Desemba 26, 2012; watu wasiojulikana wamlipiga risasi Padri
Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Michael, Mpendae mjini
Unguja na kumjeruhi vibaya.
Padri Ambros Mkenda akiwa hospitali baada ya kupigwa risasi.
Faza Mkenda alipigwa risasi nje ya nyumba yake. Alikimbizwa Hospitali
Kuu ya Mnazi Mmoja, Unguja na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili jijini Dar.
Februari 2013; Padri Evarist Mushi wa Kanisa
Katoliki Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi aliuawa kwa kupigwa risasi ya
kichwa akiwa kwenye gari akielekea kanisani kuongoza ibada.
Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi aliyeuawa kwa kupigwa risasi.
Mei 23, 2013; Sheha wa Tumondo, Mohamed Omar Said alimwagiwa tindikali
na mtu asiyejulikana. Alipata majereha sehemu ya kifuani na jicho la
kulia na kukimbizwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Unguja
ambapo alipatiwa matibabu ya dharura.
Agosti 8, 2013; wasichana
wawili raia wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kristie Trup (18) walimwagiwa
tindikali wakiwa katika matembezi ya kawaida Mtaa wa Shangani mjini
Zanzibar na kujeruhiwa sehemu za uso na kifuani.
Kate Gee na Kristie Trup waliomwagiwa tindikali wakiwa katika matembezi ya kawaida Mtaa wa Shangani mjini Zanzibar.
Kufuatia mtiririko huo, habari zinadai kuwa hali ya maisha ya Zanzibar
kwa sasa si shwari kwani viongozi wa kiimani wamekuwa wakitafakari upya
jinsi ya kuishi visiwani humo au kurudi Bara.
Yapo madai kwamba,
baadhi ya viongozi hao wa dini na raia wameingiwa hofu na wamepanga
kuandamana ili kupinga hali ya hatari inayotokana na vitendo hivyo huku
kundi moja lenye imani kali likitajwa kuhusika. Polisi bado inachunguza
matukio yote hayo.
-GPL
0 comments: