LOWASSA ATOBOA SIRI..BARAZA LA MAWAZIRI LILIMPINGA..
WAZIRI Mkuu mstaafu ambaye pia ni Mbunge
wa Monduli, Edward Lowassa, amesema Baraza la Mawaziri, lilimpinga
asisafirishe maji kutoka Ziwa Victoria hadi wilayani Kahama, Mkoa wa
Shinyanga. Amesema kwamba, siku aliyowasilisha wazo hilo katika baraza
hilo, mawaziri wote walimpinga, isipokuwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na
Mohamed Seif Khatib.
Lowassa alitoboa siri hiyo jana,
alipokuwa akizungumza katika harambee ya uchangiaji wa Shule ya Msingi
ya Kanisa la AICT, Kahama, Shiyanga.
Pamoja na hayo, alisema anayetakiwa
kupongezwa katika mradi huo ni pamoja na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa,
kwa kuwa alishiriki kuufanikisha.
“Niwapeni siri moja, nilipendekeza
waraka wa kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa Rais Mkapa, naye akaniuliza,
wale wakubwa tutawaweza? Nikamwambia tutawaweza, akauleta katika Baraza
la Mawaziri.
“Kule mawaziri wote waliupinga, kasoro
Rais Kikwete, ambaye wakati ule alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje pamoja na
rafiki yangu, Mohamed Seif Khatibu.
“Mzee Mkapa baada ya kusikiliza mawazo
yote, akaamua fedha zitolewe, na sasa mnafaidi maji safi kutoka Ziwa
Victoria,” alisema Lowassa.
Ufafanuzi huo aliutoa baada ya
Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, kumsifu Lowassa kwa
kuleta maji mkoani humo, ambapo alisema wananchi wa Shinyanga wanayaita
maji hayo kwa jina la Malowassa, yaani maji ya Lowassa.
Pamoja na hayo, wakati msafara wa
Lowassa unaingia wilayani Kahama, wananchi walijaa barabarani na
kumshangilia, huku baadhi wakionyesha maji kama ishara ya kutambua
mchango wake katika maji hayo.
Lowassa, ambaye wakati maji yanapelekwa
Shinyanga alikuwa Waziri wa Maji na Mifugo, alisema wakati alipokuwa
katika juhudi za kupinga mkataba wa zamani wa kimataifa unaoipa Misri
haki miliki ya maji ya Mto Nile unaoanzia Ziwa Victoria, alikwenda
kwenye mkutano wa maji mjini Cairo, ambako alikutana na mambo mawili
makubwa.
"Wakati nateremka pale airport, nilikuta
ulinzi wa hali ya juu sana, nikauliza iweje mimi waziri tu nipewe
ulinzi namna hii! Mwenyeji wangu akatabasamu tu.
“Siku ya pili yake, nikaenda kwenye
mkutano na waandishi wa habari, sijawahi kukutana na idadi kubwa namna
ile ya waandishi wa habari, wakati ule wao walikuwa wanamjua Mwalimu
Nyerere na timu ya Simba tu ambayo iliwafunga, sasa walitaka kumjua huyo
Lowassa ni nani mwenye jeuri na nguvu ya kutaka kutumia maji haya.
“Wakaniuliza, kwa nini nataka kutumia
maji yale wakati kuna mkataba unaozuia, nikawaambia, kule Tanzania kuna
watu wanakaa umbali wa kilomita tano tu kutoka ziwani, lakini hasa kina
mama wanalazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 20 kwenda
kutafuta maji.
“Baadaye nikawaambia, tutayachota maji
yale, mtake msitake, wakashangaa, nikaondoka na sasa mnaona faida ya
msimamo wangu," alisema.
Awali, Mgeja aliwapiga vijembe wanasiasa
wanaompiga vijembe Lowassa, kwa kusema kuna kikundi cha wanasiasa
wahuni wanaomuonea wivu Lowassa.
"Kundi hili lishindwe na lilegee kwa
jina la Yesu," alisema Mgeja, huku akishangiliwa na waumini, ambapo
alimfananisha Lowassa na mto mkubwa Kkama Ruvu na kwamba hakuna
anayeweza kukinga mikono kuzuia kasi ya maji yake.
Katika harambee hiyo, Lowassa
alichangisha zaidi ya Sh milioni 220, zikiwamo ahadi na fedha taslimu,
japokuwa malengo yalikuwa ni kupata Sh milioni 150.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: