TPA HAPAKALIKI.., MWAKYEMBE APANGUA BODI YA USIMAMIZI WA BANDARI..

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, amepangua bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa kusitisha uteuzi wa wajumbe watano wa bodi hiyo. 

Uamuzi huo umetangazwa jana, siku moja tu baada ya Mwakyembe kukutana na wafanyakazi wa TPA na kuwaahidi kufanya mabadiliko ya bodi hiyo kuondoaalichoita ni mpasuko. 

 Hata hivyo katika taarifa ya Wizara ya Uchukuzi iliyotumwa jana katika vyombo vya habari, ilielezwa kuwa wajumbe hao wameondolewa katika nyadhifa zao, ili kuondoa migongano isiyo na tija ndani ya TPA.

 Kwa mujibu wa taarifa hiyo, walioondolewa katika wadhifa wa ujumbe wa bodi hiyo ni Julius Mamiro, John Ulanga, Caroline Kavishe, Dk Hildebrand Shayo na Asha Nassoro. Mbali na wajumbe hao kuondolewa madarakani, mjumbe mmoja Dk Jabiri Bakari, amejiondoa mwenyewe baada ya ombi lake la kufanya hivyo,kukubaliwa na Dk Mwakyembe.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Dk Bakari aliomba kujiondoa mwenyewe ili aelekeze nguvu zake kuimarisha Wakala wa Serikali Mtandao Tanzania (e-Government), ambao anauongoza na uko katika hatua za awali za kuimarishwa.

 “Waziri wa Uchukuzi amekubali ombi maalum la Dk Bakari ambaye vilevile ni Mtendaji Mkuu wa wakala wa eGovernment, la kujitoa kwenye Bodi ya TPA, ili aelekeze nguvu zake zaidi kuiimarisha taasisi yake ambayo huduma zake zitanufaisha idara na taasisi zote za Serikali ikiwemo TPA,” ilieleza taarifa hiyo.

Waziri amewabakiza wajumbe wawili wa Bodi, Saidi Sauko na Jaffer Machano na kuwateuwa wajumbe wapya watatu wafuatao,” ilieleza taarifa hiyo.
 

Wajumbe wapya ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo Kisamfu na Mwakilishi wa Wafanyakazi wa TPA, ambaye hakutajwa jina.

Mabadiliko hayo yabnaendana na ahadi aliyoitoa kwa wafanyakazi wa TPA juzi, pale alipowaambia kuwa yeye ana ‘saruji’ ya kuondoa mpasuko uliopo katika bodi hiyo, na kwamba wafanyakazi hao wanastahili kuwa na mwakilishi ndani ya bodi.

Udokozi sasa umepungua hadi baadhi ya nchi kama Zimbabwe wamepongeza, sasa mpasuko huu wa bodi nitaumaliza mapema na kuanzia sasa katika bodi hiyo, kutakuwa na mjuumbe mmoja ambaye ni mwakilishi wa wafanyakazi,” alisema Mwakyembe juzi, kabla ya kutekeleza ahadi hiyo jana.


-Habari Leo

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: