SERIKALI YALEGEZA MSIMAMO KUHUSU KODI YA LINE **WAZIRI WA FEDHA AKUBALI KUWAPELEKEA WABUNGE WAJADILI UPYA


Wakati Serikali imeeleza nia yake ya kuangalia upya utozaji wa kodi ya kila mwezi kwenye laini za simu za mkononi, imeeleza pia mpango wa kufunga mtambo maalumu ili kubaini malalamiko ya kampuni za simu kudaiwa kuiba fedha za watumiaji.
Katika kile kinachoonesha kusikiliza kilio cha wananchi, Serikali imesema inapitia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau ili kuiangalia upya sheria hiyo ya kutoza kodi ya Sh 1,000 kwa kila laini kwa nia ya kuwapunguzia wananchi mzigo huo.

Serikali imetoa kauli hiyo Dar es Salaam jana kupitia kwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Fedha,  Dk  William Mgimwa walipozungumza na waandishi wa habari.

Dk  Mgimwa alisema hatua hiyo imekuja baada ya Serikali juzi kukutana na watoaji wa huduma za mawasiliano nchini waliofika kuwasilisha maoni yao juu ya tozo hiyo kwa nia ya kuwapunguzia wananchi wa hali ya chini ukali wake.

Hata hivyo alipoombwa na waandishi wa habari kuyaeleza mapendekezo yaliyotolewa na watoa huduma hao wa mawasiliano, Dk Mgimwa hakuwa tayari kuyataja hadharani zaidi ya kusema ni mapendekezo mazuri na rafiki kwa wananchi wa chini.


"Tulijadiliana nao mambo mengi ambayo yatatusaidia mbele ya safari namna tunavyoweza kupunguza makali hasa kwa watu wa kipato cha chini," alisisitiza Dk Mgimwa.
 
Alisema mbali ya maoni hayo ya watoa huduma za mawasiliano, pia Serikali imepokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari na kuona umuhimu wa kuyapitia maoni hayo na kuyatolea majibu.
 
"Serikali imepokea maoni na mapendekezo mbalimbali na sasa tunakwenda kuyafanyia kazi na baadaye tutakuwa na taarifa ya kuwaeleza wananchi ni nini tulichokiona juu ya kodi hii.


"Tunajua wananchi wa chini wanaweza kuumia lakini si nia ya Serikali kumuumiza mtu yoyote," alisema Dk Mgimwa.

Hata hivyo kutokana na suala hilo kuwa la kisheria kutokana na kupitishwa na Bunge, Dk Mgimwa alisema Serikali itatoa majibu ya nini kimekubaliwa baada ya suala hilo kurejeshwa tena bungeni na kuamulia vinginevyo.


"Suala hili ni la kisheria, jambo lolote likipita bungeni likawa sheria hata mimi Waziri siwezi kulibadilisha lazima lifuate mkondo uleule. Vikao vya Bunge vitakaa hivi karibuni na jambo hilo litajadiliwa huko," alisisitiza Dk Mgimwa.

Makato hayo ya kodi kwa kila mtumiaji wa simu ya Sh 1,000 yalitakiwa kuanza kukatwa kuanzia Julai mosi mwaka huu, lakini Dk Mgimwa alisema kuwa kodi hiyo haijaanza kukatwa kutokana na mfumo wake kutokamilika.
 
Alisema nia ya Serikali katika kodi hiyo ni kuboresha huduma za maji, umeme na barabara hasa vijijini ili wananchi wawe na uwezo wa kufikisha mazao yao haraka sokoni na kwamba kodi hiyo si pekee kwani Serikali ilipokea mapendekezo 67 ya kodi lakini  baadhi yalionekana kutotekelezeka.

"Wazo hili lilitoka katika Kamati za Bunge kwa wabunge wenyewe na sisi hatuchuji peke yetu mawazo hayo, bali kuna Kamati ya Kodi na Kamati ya Bunge lenyewe ambazo pia zilihusika katika kutoa mapendekezo ya mwisho."
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: