Ukatili uliopitiliza ....Ndugu wataka MTOTO auawe
MTOTO
aitwaye Mwajuma Haji (16) ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili anayesumbuliwa na ugonjwa wa kusinyaa kwa viungo yuko katika
hali mbaya baada ya baadhi ya ndugu kudaiwa kutaka auawe ili kutoa
uchuro katika familia. Kwa
mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo, Tatu Musa baadhi ya ndugu (siyo
wote) wamekata tamaa ya kumuuguza mtoto huyo na kupendekeza heri mtoto
huyo akatishwe maisha yake.
“Mwanangu
haumwi wala hajawahi kuumwa ila ghafla alianza kusinyaa na kukosa
nguvu, kinachoniuma baadhi ya ndugu zangu wamekata tamaa wanataka
wamuue, waniachie mwanangu,” alisema mama huyo huku akilia mfululizo.
Mwandishi wetu amemshudia mtoto huyo akiwa amesinyaa viungo kiasi cha kutoweza kufanya kitu chochote zaidi ya kulala.
Mama
mzazi wa mtoto huyo alisema kuwa alijifungua mtoto huyo akiwa na afya
njema lakini alipofikisha umri wa miaka mitatu hali ikabadilika na
viungo vyake kuanza kusinyaa.
Mama
huyo amedai kwamba kutokana na hali hiyo hakuweza tena kufanya shuguli
za kumwingizia kipato zaidi ya kukaa na mwanaye kijijini kwao,
Kiamange, Bagamayo mkoani Pwani bila ya kupata matibabu ya uhakika.
Alisema kwamba maisha ya mtoto wake yameendelea kuwa mabaya bila ya
kupata msaidizi kutokana kutengwa na baadhi ya ndugu zake waliokata
tamaa ya kumuuguza.
Aidha, Mama Mwajuma amedai kwamba kuna wakati alikuwa akimfungia ndani
mwanaye kuanzia asubuhi ili aende kulima na kupata chochote, lakini
aliporudi nyumbani alimkuta katika hali mbaya sana.
Kutokana
na mazingira kuwa magumu, mama huyo alidai kwamba hakuwa na msaidizi wa
kuweza kumwachia mwanaye ili aweze kuhangaikia kipato.
Mbali
na mtoto huyo, mama huyo alibahatika kupata mtoto mwingine ambaye sasa
ana umri wa mwaka mmoja na nusu lakini baada ya kujifungua mwanaye
mkubwa akatokwa na vidonda mgongoni.
Baada ya mtoto huyo kusumbuliwa na ugonjwa huo kwa muda mrefu
alishauriwa kumpeleka Muhimbili na kumuacha mwanaye mdogo kwa majirani.
Baada ya muda alipata taarifa kwamba mtoto wake mdogo anaumwa, ikabidi
akamchukue na kumleta Muhimbili ili aishi naye ingawaje hairuhusiwi kwa
mtoto kuishi wodini.
“Nina wakati mgumu, kwa kuwa nina watoto wawili sina cha kufanya kwa
kuwa huyu mwingine hajiwezi kwa chochote zaidi ya kumsaidia kwa kila
kitu, mbaya zaidi ndugu wamenitenga,” alisema huku akibubujikwa
machozi.
Ndugu Mtanzania mama Mwajuma yuko katika hali mbaya sana, kama unataka
kumsaidia mtoto wake tuma mchango wako kupitia namba 0754 021 301.
0 comments: