REGNALD MENGI NA WAZIRI SOSPETER MUHONGO WASHIKANA MASHATI...


MWENYEKITI Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wameingia katika mzozo mzito kuhusu uwekezaji katika sekta ya gesi.

Katika mzozo huo, Mengi amemshambulia Waziri Muhongo kwa kumwita ni mwongo, mpotoshaji na mwenye lengo la kuwatoa Watanzania kwenye hoja ya msingi ya rasilimali yao ya gesi.

Mengi alitoa kauli hiyo jana kupitia taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari mbalimbali nchini.

Mzozo wa vigogo hao ulianza wiki mbili zilizopita baada ya Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa taasisi ya Uwekezaji nchini (TPSF), kukutana na waandishi wa habari na kueleza msimamo wa taasisi hiyo katika suala la uwekezaji wa gesi nchini.

Katika maoni yake, TPSF ilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi na kuishauri serikali kusitisha ugawaji wa vitalu vya gesi hadi sera ya gesi itakapokuwa tayari na taasisi hiyo iliomba kukutana na Waziri Muhongo kwa majadiliano zaidi.

Baada ya ushauri huo, Waziri Muhongo alijibu kupitia vyombo vya habari kwamba mpango wa kugawa vitalu vya gesi na kuingia mikataba uko palepale kama ulivyopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Prof. Muhongo pia alitamka bila kumng’unya maneno kwamba hana mpango wa kukutana na TPSF, kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda, na kuongeza kuwa uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania ni kuwekeza kwenye soda na juisi, si kwenye sekta ya gesi.

Septemba 7, mwaka huu, mzozo huo uliingia katika hatua mbaya zaidi baada ya mtu aliyejitambulisha kwa jina la ‘CCM Tanzania’, kusambaza taarifa kwa njia ya barua pepe kwa vyombo vyote vya habari na kumshambulia Mengi kwa kumwita fisadi, mbinafsi na mfitini wa maendeleo.

‘CCM Tanzania’ kama anavyojiita, alidai katika barua pepe yake kuwa Mengi amepanga kuwatumia vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanya kongamano lenye maudhui: ‘Rasilimali za nchi na manufaa kwa wazalendo.’

Alisema kongamano hilo limepangwa kupewa muda maalumu na Kituo cha Televisheni cha ITV kinachomilikiwa na Mengi na lengo lake ni kutaka kuionesha jamii kuwa Waziri Muhongo na watendaji wengine wa wizara hiyo hawajali masilahi ya wazawa na hawana utaifa wala uzalendo.

‘CCM Tanzania’ alisema si mara ya kwanza kwa sekeseke la aina hii kuzuka ama kuzushwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mengi na mara zote amekuwa akitumia nguvu ya ushawishi wa vyombo vya habari anavyovimiliki katika kutafuta kuungwa mkono na hata kuonesha ubaya wa wabaya wake.

Akijibu tuhuma hizo kupitia taarifa yake jana, Mengi alisema Septemba 7, mwaka huu, alipokea barua pepe yenye kichwa cha habari kisemacho: “Ubinafsi/ufisadi wa Mengi na chuki/ fitna kwenye maendeleo.”

Alisema aliyetuma barua pepe hiyo ambayo Tanzania Daima ina nakala yake, alijitambulisha kama ‘CCM Tanzania’ na aliisambaza kwa vyombo mbalimbali vya habari, wanasiasa na watu wengine wa kada mbalimbali.

“Kabla ya barua pepe hiyo, nilifowadiwa pia nakala ya ujumbe (sms) na watu ambao walitumiwa na Prof. Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na mbunge inayosema:

“Wambieni Watanzania: Kampuni za Mengi zimeshikilia vitalu 59 vya madini vyenye ukubwa wa mita za mraba 3,752.37 (sq km) amevishikilia, ameshindwa kuviendeleza. 
 
Watanzania wanakosa mapato na ajira! Sasa anataka vitalu vya gesi na mafuta. Je, huu ndio uzawa?

“Mengi hana uzawa bali ubinafsi. Anataka kufanya udalali wa vitalu vya rasilimali zetu. Waelezeni Watanzania ukweli huu,” alisema.

Mengi katika taarifa yake hiyo, aliendelea kusema kuwa mbali ya Waziri Muhongo kutuma ujumbe huo, vilevile Septemba 5, alijibu kwa dharau swali la mwandishi wa habari lililouliza:
 
“Waziri tunataka ufafanuzi kuhusu kauli yako ya hivi karibuni kwamba Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika uwekezaji wa gesi asilia. Kwanza, kauli hii ni kweli? Pili, kauli kwamba Watanzania wanaweza kuwekeza kwenye sekta ya machungwa tu, huoni si kwamba unawavunja moyo bali unawadhalilisha wawekezaji wazalendo?”
 
Alisema kuwa Prof. Muhongo alijibu: “Kila mtu alitoa mawazo ya sera ya gesi wakiwamo TPSF. Mengi na wenzake wanataka vitalu wafanye ulanguzi wa gesi na mafuta yetu. Tutatoa orodha ya vitalu vya madini vilivyoko mikononi mwa Mengi ambavyo anafanya ulanguzi. Ukweli utaonyesha ubabaishaji na ulanguzi wa Mengi wa genge lake.”
 
Mengi alisema ameona ni bora atumie haki yake ya kujibu na kuwaonya wanaohusika kusambaza taarifa hizo kuchafua jina lake, wajue kwamba atawachukulia hatua za kisheria.
 
Kuhusu kusingiziwa kwa vitalu vya madini katika hoja ya gesi, alisema huo ni upotoshaji na uongo wa hali ya juu wa Waziri Muhongo, wenye lengo la kuwatoa Watanzania kwenye hoja ya msingi ya rasilimali yao ya gesi, kwani hajawahi kufanya udalali kwenye vitalu vya madini.
 
Alisema tamko la TPSF, lilitokana na kikao cha bodi ya taasisi hiyo cha Agosti 28 na baadaye kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Alisema mambo mengi yalizungumzwa katika kikao hicho, ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa Watanzania (Economic Empowerment) na mambo muhimu matatu yalijadiliwa na kutolewa mapendekezo.

Mengi aliyataja mambo hayo kuwa ni kuhusu manunuzi ya umma (public procurement), ardhi na uvuvi na tatu, ni suala la gesi asilia.

“Kwenye mkutano na waandishi wa habari, mimi nikiwa Mwenyekiti wa TPSF, niliwasilisha maoni ya TPSF kuhusiana na manunuzi ya umma, wakati Makamu Mwenyekiti wangu, Salum Shamte, aliwasilisha maoni yetu kuhusiana na sekta ya ardhi na uvuvi na mwishoni Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, aliwasilisha maoni ya TPSF kuhusiana na gesi asilia.

“Katika maoni yetu, TPSF ilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi na kushauri kusitishwa ugawaji wa vitalu vya gesi hadi hapo sera ya gesi itakapokuwa tayari. Mwisho, Bwana Simbeye alisema kwamba TPSF itaomba kukutana na Profesa Muhongo kuwasilisha mawazo na mapendekezo ya taasisi hiyo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mengi, matokeo yake Prof. Muhongo hajajibu hoja na badala yake alitoa majibu ya kumshambulia mwenyekiti huyo.

“Binafsi nilishitushwa na msimamo wa Prof. Muhongo, kwani Serikali ya Awamu ya Nne imepiga hatua kubwa katika kudhihirisha kuwa ni “serikali sikivu”. Ingemgharimu nini Prof. Muhongo kukaa na kutusikiliza? Hakuna ambacho angepoteza zaidi ya dakika chache za muda wake.

“Jambo la pili ambalo lilitokea ni mimi binafsi kushambuliwa kana kwamba maoni yaliyotolewa kuhusiana na gesi ni maoni yangu binafsi na si ya TPSF. Mifano ya mashambulizi dhidi yangu ni kama nilivyoonyesha hapo juu katika email na ujumbe mfupi wa simu (sms),” alisema.

Msimamo wa Muhongo
Katika taarifa hiyo, Mengi alishangazwa na undumila kuwili wa Prof. Muhongo katika suala la uwekezaji wa gesi.

Alisema, mara baada ya Muhongo kuingia wizarani alisema kinaga ubaga kwamba sheria iliyopo haikidhi mahitaji ya sekta ya gesi asilia ndiyo maana akasimamisha ugawaji wa vitalu vya gesi na kuamrisha mikataba ipitiwe upya na sera ipatikane.

“Leo tunashuhudia Prof. Muhongo akila matapishi yake na kusema kwamba sheria zile zile alizoziponda sasa zinafaa,” alisema.

Alisema msimamo wa Prof. Muhongo kuhusu uwekezaji wa gesi mara baada ya kuteuliwa kuwa waziri ulikuwa ni kutaka kupitishwa kwanza kwa sera ya gesi asilia kabla ya kuendelea na ugawaji wa vitalu vya gesi.

Alisema hii imejionesha katika kauli ya Muhongo Septemba 2012 ambapo alikaririwa akisema: “Baadhi ya mikataba ni ya ovyo, na inahitaji kuvunjwa.” Na “Sitovumilia mikataba ambayo haina masilahi kwa nchi na inawanufaisha wachache.”

Baada ya hapo, Profesa Muhongo aliamrisha Bodi mpya ya TPDC kusitisha ugawaji wa vitalu vya gesi ambao ulipangwa kufanyika Septemba 2012 na kupitia upya mikataba yote.

Kwa mujibu wa Mengi, baada ya kauli hii ya Waziri Muhungo, zoezi la kugawa vitalu vya gesi asilia lilisitishwa lakini hadi sasa matokeo ya kupitia upya mikataba hayajatolewa hadharani.

Alisema miezi michache baadaye, Februari 26, 2013, Profesa Muhongo alisisitiza msimamo wake wa kutaka Tanzania kuwa na sera ya gesi kabla ya kugawa vitalu zaidi.

Aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano uliofanyika Chatham House, mjini London. Mkutano huo ulipewa jina “Tanzania: An Emerging Energy Producer”.

Mengi alisema jambo la kushangaza, Profesa Muhongo amebadilika na sasa anataka vitalu vigawiwe kabla ya kuwapo kwa sera ya gesi.

Alisema Prof. Muhongo amenukuliwa na gazeti la Daily News la Agosti 31, 2013 akieleza sababu zake za kutaka vitalu vigawanywe kabla ya kupitishwa kwa sera ya gesi ambazo hazina mashiko.

“Sababu kuu alizozisema Muhongo kubadili msimamo wake ni tatu; mosi, ushindani wa soko na majirani zetu, akitolea mfano wa Msumbiji. Pili, sheria ya mwaka 1960 iliyoanzisha TPDC na Sheria ya Petroli ya mwaka 1980, kwamba zinatosha kusimamia ugawaji wa vitalu, akimaanisha sera na sheria mpya zitafuata baada ya ugawaji wa vitalu; na tatu, Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika sekta hii akimaanisha waachiwe wageni peke yao,” alisema Mengi.
 
Alisema kauli ya Prof. Muhongo kwamba wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza tu kushiriki biashara ya juisi na soda na hawana uwezo wa kushiriki katika biashara ya gesi yao ni dharau.

“Kigezo gani Profesa Muhongo anatumia kutoa kauli ya jumla yenye kutawaliwa na hisia? Amefanya utafiti gani kupima uwezo wa kifedha wa wafanyabiashara wa Kitanzania? Kwa taarifa yake, wapo wafanyabiashara wengi ambao wanaweza kupata fedha kwa ajili ya kuchimba visima vya gesi,” alisema Mengi.

Akijibu barua pepe ya mtu aliyejiita ‘CCM Tanzania’, aliyesema Mengi si mzalendo, Mwenyekiti huyo alisema Watanzania ndio wanaojua uzalendo wake.

“Ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi si mzalendo Wantanzania wanafahamu ukweli. Vilevile ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi ni mbinafsi na sipendi maendeleo ya Watanzania wenzangu kwa hili pia Watanzania wanafahamu ukweli,” alisema.

Alisisitiza kuwa hapingi uwepo wa wawekezaje wageni katika sekta ya gesi lakini kuna mambo mawili anapigania; mosi, Watanzania wanufaike na rasilimali yao ya gesi na pili, iwepo sera ya gesi inayotoa kipaumbele kwa Watanzania.

Mimi napenda maendeleo ya nchi yangu; kwa hiyo hata siku moja siwezi kupinga uwekezaji ama ubia na wawekezaji. Ninachosimamia ni manufaa kwa nchi yangu.
-Tanzania daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: