RAISI KIKWETE NA KAGAME WAMALIZA TOFAUTI ZAO NA KUKUBALIANA KUSHIRIKIANA KAMA ZAMANI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Septemba 5, 2013, amekutana kwa faragha na Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame katika mazungumzo yaliyokwenda vizuri na kuwaridhisha viongozi hao wawili wa nchi jirani. 

Viongozi hao wamekutana kwa zaidi kidogo ya saa moja katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa Kampala, Uganda. 

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Rais Kagame wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili

Viongozi hao wawili wako nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Maziwa Makuu – “International Conference on the Great Lakes Region (ICGLR)” unaofanyika leo Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort. 

Viongozi wengine ambao wanahudhuria Mkutano huo ni pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR na mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Silva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU). 

Rais Kikwete na ujumbe wake amewasili Kampala asubuhi ya leo akitokea mjini Dodoma ambako aliwasili jana jioni kwa ajili ya hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuuu wawili iliyofanyika Ikulu Ndogo, Dodoma. 
 
Rais Kikwete aliwasili Dodoma akitokea Mwanza ambako alihudhuria mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu Mkuu Dkt. Moses Samwel Kulola yaliyofanyika kwenye Kanisa la Bugando Calvary Temple, mjini Mwanza. 
 
Imetolewa na;
 Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, 
Ikulu, 
DAR ES SALAAM. 
 05 Septemba, 2013 
---------------------
 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Rais Paul Kagame wa Rwanda wakati walipokutana faragha sambamba na mkutano wa wakuu wa nchi za Maziwa Makuu uliofanyika katika Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, jijini Kampala,Uganda, leo
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika mazungumzo na Marais Paul Kagame wa Rwanda(kushoto), Rais Salva Kiir wa Sudan ya kusini na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda 
Baadhi ya viongozi wan chi za jumuiya ya Maziwa Makuu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mkutano wa wakuu wa nchi hizo uliofanyika jijini Kampala Uganda leo.Kutoka kushoto ni Rais Salva Kiir wa Sudani ya Kusini,Rais Joseph Kabila wa DRC,Rais Dkt.Jakaya Kikwete,Rais Yoweri Museveni wa Uganda,Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Dkt.Nkosazana Dlamini Zuma na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Rais Paul Kagame wa Rwanda wakati walipokutana na kufanya mazungumzo ya faragha, katika Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, jijini Kampala
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: