RAISI KIKWETE ASHANGAZWA NA KIASI KIKUBWA CHA UONGO WA WAPINZANI KWA WATANZANIA..
RAIS Kikwete, amesema anashangazwa na kiwango cha uongo cha baadhi ya
wanasiasa ambao hakuwataja majina, kuwa wamekuwa wakizusha madai kuwa
Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, bila kuongozwa na
mapendekezo ya wadau mbalimbali waliopendekeza majina hayo.
Alisema
bado anaendelea kuamini mchakato wa Katiba mpya utafikia mwisho wake
mwaka 2014 na hivyo kuiwezesha Tanzania kufanya uchaguzi mkuu wa mwaka
2015, chini ya Katiba mpya.
Alisema
hana tatizo na watu wanaopinga sera za serikali ama hata kumpinga yeye
binafsi, bali tatizo lake ni wanasiasa na wanaharakati wanaochochea
ghasia, fujo na uvunjifu wa amani.
Rais
Kikwete, aliyasema hayo juzi, mjini San Rafael, California, nchini
Marekani, wakati alipokutana na kuzungumza na jumuia ya Watanzania
waishio katika Jimbo la California.
Katika
hotuba yake, ambayo alizungumzia mambo mbalimbali, Rais Kikwete
aligusia mjadala wa karibuni bungeni kuhusu mchakato wa Katiba mpya na
kusema kuwa alishangazwa na madai kuwa yeye kama Rais, hakuongozwa na
mapendekezo ya wadau wakati anateua Tume ya Katiba.
“Watu
wote niliowateua walipendekezwa na wadau mbalimbali, zikiwamo taasisi
za dini. Yule Mama Maria Kashonda alipendekezwa na Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC), Mama Mwantumu Malale alipendekeza na Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (BAKWATA). Kila kundi ambalo lilipendekeza watu
limepata mjumbe katika tume hiyo, wakiwemo walemavu ambao naambiwa
nimewasahau,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
Kuhusu kama Tanzania itaweza kupata Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais Kikwete alisema:
“Ningependa
sana na kwa kweli ni matarajio yangu makubwa, tuweze kumaliza mchakato
wetu mwaka 2014 na tuweza kuwa na Katiba Mpya ili iongoze Uchaguzi Mkuu
wetu wa mwaka 2015. Mchakato wetu unakwenda vizuri na wala siyo lazima
tuhangaike na Katiba kwa miaka mingi. Muhimu ni ushirikishwaji wa kila
mmoja wetu.”
Akizungumzia
tabia za wanasiasa wa Tanzania kwa jumla, hasa wale wanaochochea chuki
na ghasia, Rais Kikwete aliwaambia Watanzania hao:
“Sina
tatizo na wanasiasa ama wanaharakati kupinga sera za Serikali yangu.
Hili ni suala la nguvu ya hoja na tunao uwezo mkubwa sana wa kutetea
sera zetu. Na wala sina tatizo na watu kunipinga mimi binafsi.
Kinachonipa taabu mimi ni pale wanasiasa na wanaharakati wanapochochea
ghasia na kuleta fujo. Kama mtu anataka kuongoza Tanzania si asubiri
hadi atakapochaguliwa?”
Aliongeza
Rais Kikwete: “Hivi unapochochea ghasia, fujo na chuki na kweli mambo
hayo yakatokea na nchi ikateketea, utaongoza nchi ya namna gani?
Utaongoza magofu na majivu yatakayobakia baada ya nchi kuteketea?”
Kuhusu
mjadala wa karibuni kuhusu kama Rais awe na madaraka ya kuteua wajumbe
166 wa nyongeza ili kuingia katika Bunge la Katiba kujadili Rasimu ya
Katiba Mpya, Rais Kikwete amesema kuwa yeye hana tabu kama itabidi ateua
basi atateua, lakini kama siyo lazima yeye hana tabu.
DAWA ZA KULEVYA
Katika
hatua nyingine, Rais Kikwete amesema Serikali yake haitawatetea
Watanzania wanaokamatwa wamebeba dawa za kulevya nje ya nchi kwa sababu
biashara hiyo ni haramu na ni uvunjaji wa sheria.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu,
mjini Dar es Salaam jana, ilisema Rais Kikwete alisema ni wajibu wa
Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema na kufuata na kuheshimu
sheria katika nchi wanamoishi kwa sababu wakivunja sheria za nchi hizo,
Serikali yake haitawatetea.
Akizungumza
na Watanzania hao katika Hoteli ya Embassy, iliyoko San Rafael, Rais
Kikwete alikiri Watanzania wengi kujiingiza kwa kiasi kikubwa katika
biashara za ovyo ovyo kama za dawa za kulevya, lakini Serikali yake
haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakishiriki biashara hiyo.
“Ukikamatwa
na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi zetu,
zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya
biashara za ovyo ovyo kiasi hiki. Serikali itawatetea Watanzania
wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa
za kulevya ama kubaka watu hatukutetei kamwe,” alisema Rais Kikwete.
Miongoni
mwa Watanzania wanaoshikiliwa nje ya nchi kwa kukamatwa na dawa za
kulevya ni pamoja na Agness Masogange na Mellisa Edward ambao
wanashikiliwa nchini Afrika Kusini.
Watanzania
hao, walikamatwa Afrika Kusini kwa madai ya kusafirisha kilo 150 za
dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine, wakati wakitokea nchini
Tanzania.
Watanzania
wengine wanaoshikiliwa nje ni bondia maarufu Mbwana Matumla (Hispania),
nyota wa zamani wa timu ya Simba, Joseph Kaniki na bondia Mkwanda
Matumla, ambao wanashikiliwa nchini Ethiopia.
-Mtanzania & freebongo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: