HIZI NDO SABABU ZA RWANDA KUIKACHA BANDARI YA DAR ...
SIRI ya wateja wakubwa wanaotumia
Bandari ya Dar es Salaam, wakiwemo wa nchi jirani kama Rwanda kutishia
kujitoa na kwenda kutumia bandari za nchi nyingine, imefahamika,
Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Siri hiyo inaelezwa kusababishwa na
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuwa na mpango wa kuanzisha tozo mpya
kuanzia Oktoba mwaka huu kwa wateja wanaoingiza mizigo yao nchini
pamoja na kasi ndogo ya utendaji ukilinganisha na bandari za nchi
jirani.
Tozo hiyo mpya inayopigwa ni ya ufuatiliaji mizigo bandarini kwa njia ya mtandao (Electronic Cargo Tracking Note).
Hatua ya Rais Kagame kuikacha Bandari ya
Dar es Salaam kunadaiwa kusababishwa na kulegalega kwa mahusiano kati
ya Tanzania na Rwanda, lakini duru za siasa zinabainisha kuwa rais huyo
alishaitahadhalisha serikali kuboresha utendaji wa TPA na kupunguza
vikwanzo vya kibiashara kutoka 24 hadi 12.
Imeelezwa kwamba tozo hiyo ya e-CTN
itaathiri mapato ya bandari za Tanzania kutokana na kuwa washindani wake
wote hawana tozo hizo ikiwamo bandari za Mombasa, Walvis bay, Nacala,
Maputo na Durban, ambazo zimekuwa zikichukua wateja wengi wa bandari za
Tanzania wakiwamo wale wa nchi za Burundi, Rwanda, Zambia, DRC na
Malawi.
Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa kodi
hiyo imeibua utata mkubwa baada ya kuwapo njama za kulazimisha kuwapo
kwake pamoja na pingamizi kutoka kwa wadau na hata baadhi ya watendaji
serikalini.
Taarifa za uhakika ndani ya mfumo wa
bandari zilizothibitishwa na baadhi ya wadau, zinaeleza kwamba TPA ambao
wamekwisha kuingia mkataba na kampuni moja ya Ubelgiji, iitwayo Antaser
BVBA imeendelea na mchakato wa kuanzisha tozo hiyo.
Pamoja na pingamizi kutoka kwa wadau na
hata ndani ya TPA yenyewe, bado kuna taarifa za kwamba uongozi wa
mamlaka hiyo unaendelea na mchakato wa kuanza tozo hiyo ya e-CTN Oktoba
mosi mwaka huu na baadhi ya watendaji wake wanapanga kwenda Ubelgiji
kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya utekelezaji wake.
Tozo hiyo ya e-CTN ni kwa ajili ya
ufuatiliaji wa mzigo kutoka nchi inakotoka kwa njia ya mtandao, kazi
ambayo wadau wanasema hufanywa na kampuni za meli na zile za wakala
wanaosafirisha mizigo hiyo na si dhamana ya TPA ambao jukumu lao ni
kupokea mizigo kutoka kwenye meli (cargo handling) na kuifadhi kwa muda
ikisuburi wateja kuichukuwa.
“TPA walitakiwa wawasilishe pendekezo
hili la e-TCN kwa Sumatra ambao kwa mamlaka waliyonayo wawaite wadau
wote watoe mapendekezo yao kama uwepo wa kitu kama hiki utaleta tija kwa
wadau wote wanaotumia bandari ya Dar es salaam. Kutokana na hila na
pengine ufisadi uliojificha ndani. Gharama zake zitakwenda kwa mlaji wa
mwisho! TPA kazi yake ni kupokea mizigo kutoka kwenye meli (Cargo
handling) na kuifadhi kwa muda ikisuburi wateja waje kuichukuwa aidha
wao wenyewe au kwa kutumia mawakala wao wa forodha.
“TPA wanatakiwa ku kuibana mizigo ikiwa
ndani ya bandari na si kutoka bandari nyingine duniani ( ports of
loadings) mpaka final destination ya mizigo bila " carriers" yaani
shipping lines/ agents kuhusika na pia wenye mizigo (Cargo Owners) yaani
importers/ C&F agents kuhusishwa!!. Hapa kuna kitu
kilichojificha,” anasema mdau ambaye anafanya biashara ya uwakala wa
meli.
Tayari kumeibuka utata kuhusiana na huo
mradi wa Electronic Cargo Tracking Note baada ya wadau kushitukia njama
za kuwazunguka kwa njia ya kughushi muhstasari wa kikao wenye nia ya
kuhalalisha mradi huo.
Utata huo umeibuka baada ya wadau
kubaini kuwapo kwa kikao kilichofanyika Mei 30, 2013 kikiwashirikisha
baadhi yao na baadaye kuandika muhstasari (nakala tunayo) ambao
uliandikwa majina ya watu ambao hawakuhudhuria akiwamo Mwenyekiti,
Otieno Igogo.
Igogo alibaini kuwapo kwa njama hizo na
baadaye ‘kuvamia’ kikao kingine kilichoitishwa bila ya yeye kualikwa
kilichofanyikia Agosti 29, 2013, ambacho alikiongoza na kutamka wazi
kuwa jina lake pamoja na baadhi ya hoja za kikao cha Mei 30, 2013
vilighushiwa na hivyo kwa kauli moja wajumbe kufanyia marekebisho
muhtasari.
Miongoni mwa hoja zilizoghushiwa katika
muhtasari wa kikao hicho ni hoja ya kwamba wajumbe walijadili na
kuridhia mpango wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuanzisha tozo kwa
ajili ya huduma za Electronic Cargo Tracking Note (e-CTN), na katika
kikao cha wiki hii, wadau walirekebisha muhtasari huo na kukemea
waliohusika na kughushi.
Mwakilishi wa Chama cha Mawakala wa Meli
(TASAA), Paul Kirigini, ambaye ni mjumbe wa vikao hivyo alithibitisha
kuwapo kwa tatizo katika muhtasari wa kikao cha Mei 30, 2013 ambao
uliandaliwa katika mazingira tata kwa kuorodhesha watu ambao
hawakuhudhuria na baadhi kuandika kwamba waliomba udhuru wakati hawakuwa
wamealikwa akiwamo yeye.
“Mimi sikualikwa lakini wameandika
kwamba sikuhudhuria kwa kuomba udhuru. Nilikuwapo Dar es Salaam na hata
kama nisingekuwapo tungetuma mwakilishi wa TASAA, lakini hawakutuita na
wakaandika kwamba tuliomba udhuru. Kibaya zaidi hata Igogo ambaye
alipaswa kuwa mwenyekiti wa kikao hicho hakuwapo lakini wakaandika ndiye
aliendesha hicho kikao,” anasema Kirigini.
Igogo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati
Ndogo ya Wadau wa Bandari, hakuweza kupatikana jana kuzungumzia sakata
hilo, lakini ilielezwa kwamba ameridhika baada ya muhtasari huo
kufanyiwa marekebisho na kuazimiwa kwamba vikao vyote lazima wadau
wajulishwe kabla ya kuitishwa.
Mjumbe mwingine ambaye anatajwa jina
lake kuingizwa bila ya yeye kuwapo ni Stephen Ngatunga, ambaye naye
aliomba kufanyika kwa marekebisho hayo katika kikao cha Alhamisi wiki
hii.
Mwakilishi wa TPA, ambaye ni Kaimu
Mkurugenzi wa Teknohama, Phares Magesa, anaelezwa kuwa ndiye
aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wake, Madeni Kipande, ambaye hata vikao
vilivyoitishwa na SUMATRA alishindwa kuhudhuria.
Mara baada ya kutokea malalamiko
kuhusiana na Electronic Cargo Tracking Note, wadau walilazimisha
kuitishwa kwa kikao kilichoongozwa na SUMATRA, lakini uongozi wa TPA
ulishindwa kuhudhuria vikao vilivyoitishwa Julai 17 na Julai 22 mwaka
huu.
Katika vikao hivyo viwili vya Julai,
SUMATRA iliungana na wadau kuitaka TPA kuwashirikisha kabla ya kufikia
maamuzi ya kuingiza tozo zozote zitakazoweza kuathiri wateja wanaotumia
bandari za Tanzania ikiwamo bandari ya Dar es Salaam.
Mradi huo wa e-CTN unaelezwa na wadau
kuweza kupandisha gharama za uingizaji wa mizigo bandarini hadi kufikia
dola milioni 100 kwa mwaka kwa kutumia takwimu za mizigo ya makontena
kwa mwaka 2012, ukiondoa mizigo mingine kama magari, nafaka na mafuta.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
ameshaingilia kati changamoto ndani ya Bandari ya Dar es Salaam na
aliitisha kikao cha wadau kilichoahirishwa ghafla kutokana na
kuingiliana na majukumu mengine ya kitaifa.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: