Professa
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ramadhani Senzota, anashikiliwa na
Jeshi la Polisi kwa kosa la kumjeruhi kwa risasi fundi ujenzi,
aliyefahamika kwa jina la Fadhili Mkachini.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema
tukio hilo lilitokea juzi saa 10:50 jioni eneo la Tegeta Salasala,
wakati Fadhili na mafundi wenzake wakiendelea na ujenzi.
Kamanda Kova alisema tukio hilo lilitokea baada ya mafundi hao
wakiendelea na ujenzi wa nyumba ya mtu anayetambulika kwa jina la
Khadija, ndipo Profesa huyo alitokea na kuwataka wasitishe shughuli
hiyo.
Kova alisema kabla ya mafundi hao kufanya chochote, Profesa huyo
alichomoa bastora aina ya Akidali Mini yenye namba 03 TZ CR 92277,
iliyokuwa na risasi saba ndani ya magazine na kumpiga fundi huyo
tumboni na kumsababishia maumivu makali.
Hata hivyo, Profesa Senzota anashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi
na fundi huyo amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala akipatiwa
matibabu.
Wakati huo huo, watu saba wanaosadikiwa kuwa majambazi wanashikiliwa na
Polisi kwa kufanya uhalifu wa kutumia silaha, sare za polisi na redio ya
mawasiliano katika maeneo ya Boko, Tegeta, Mbweni, Bahari Beach na
maeneo mengine ya Jiji.
Watuhumiwa hao ni Khamis Mkalikwa (40), Magila Werema (31), Nurdin
Bakari (46), Materu Marko (32), Louis Magoda (34), Amos Enock (23) na
Amir Mohamed (45), wote wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Kamanda Kova alisema watuhumiwa hao walikamatwa jana katika eneo la
Kiluvya, Wilaya ya Kinondoni na walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota
Cresta GX 100, yenye namba za usajili T 546 BWR.
Baada ya kukamatwa watuhumiwa hao walikutwa na bastora moja aina ya
Brown B.3901, ambayo ilikutwa na risasi nne na ganda moja la risasi,
sare za polisi pea mbili na moja yenye cheo cha Stesheni Sajenti na
nyingine ikiwa na beji inayosomeka kwa jina la SSGT A.M.Mduvike.
Kova alisema watuhumiwa wawili kati ya saba wamejeruhiwa na wapo hospitali kwa matibabu na uchunguzi dhidi yao bado unaendelea.
Katika tukio lingine, mtu aliyetambulika kwa jina la Alquine Masubo
(42), anashikiliwa na polisi kwa kosa la kujifanya Ofisa Usalama wa
Taifa.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa na vielelezo mbalimbali ikiwamo kitambulisho
cha JWTZ namba 7001-E.1075, bastola aina ya Browning yenye namba
A.956188-CZ83 ikiwa na risasi 12 ndani ya magazine, pia alipekuliwa
nyumbani kwake na kukutwa na bastola nyingine aina ya MAKNOV yenye namba
BA4799 ikiwa na risasi 19 na bastola moja ilikuwa na umiliki na
nyingine ilikuwa haina.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: