LIPUMBA AIPONDA SEREKALI YA CCM NA KUDAI IMESHINDWA KAZI...
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba ametupa kombora kwa Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), akisema imeshindwa kutekeleza ahadi zake na badala yake
inatumia vyombo vya dola kuwakandamiza na kuwaumiza wananchi.
Lipumba pia aliishutumu Serikali kwa
kuwakumbatia viongozi ambao wanatuhuma za ubadhilifu kwa kuwahamisha
katika vituo vyao vya kazi, hivyo kuendelea kuzorotesha uchumi wa nchi
na kusababisha hali ya ugumu wa maisha kwa wananchi.
Aliyasema hayo jana wakati akifugua
mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho, Dar es Salaam, ambapo alisisitiza
kuwa ubadhilifu ambao unakumbatiwa na Serikali hiyo umedhihirishwa pia
na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mtaa (LAAC)ambayo imebaini
kuwapo mtandao unaohusisha viongozi wa Serikali wanaotafuna fedha za
umma.
“Hii ni Serikali ya kisanii sana maana kila inachokisema haitekelezi kwa mfano kule Mtwara wananchi wanaendelea kuteswa .
Alisema Serikali imeshindwa kutekeleza ilani yake ikiwamo kuwapatia maisha bora wananchi.
Profesa Lipumba pia alieleza
kusikitishwa kwake na nguvu kubwa iliyotumika katika kumkamata Kiongozi
wa Jumuiya ya Taasisi ya Kiislam Sheikh Issa Ponda, akidai kuwa licha ya
kwamba naye kuna wakati huwa haungi mkono kauli zake, lakini haoni kama
ni sahihi kumhukumu kwa kumshambulia kwa risasi.
Alisema hatua yake ya kuzungumzia mara
kwa mara suala la Sheikh Ponda haimaanishi kuwa anafanya hivyo kwa kuwa
ni Mwislamu mwenzake, bali anafanya hivyo kwa kutambua ni wajibu wake
kutetea haki kwa wananchi wote.
Alisema ni wajibu wake kukemea na
kulaani vitendo kama hivyo akisema vilianza kwa Mwandishi wa Habari wa
Channel Ten, Mwangosi, vikafuata kwa Ponda na kwamba kesho vinaweza
kumkuta yeye.
Kuhusu mchakato wa maoni kwenye Katiba
Mpya, Profesa Lipumba, alikosoa akisema kuwa baadhi ya vipengele
havijafafanua bayana kuhusu muundo wa Serikali na namna inavyoweza
kujiendesha.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: