Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amehoji kesi 36 zinazohusiana na
dawa za kulevya ambazo Jeshi la Polisi limekaa kimya kwa kutoeleza hatua
zilipofikia, hali ambayo inatia shaka na kudhoofisha vita dhidi ya
biashara hiyo haramu.
Alisema hayo juzi wakati akihojiwa na televisheni ya Channel Ten kuhusu
serikali imejipanga vipi kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya
ambayo inaonekana kukithiri nchini na kuathiri asilimia kubwa ya vijana.
Dk. Mwakyembe alisema ili Watanzania wafahamu nini kinachoendelea
kuhusiana na kesi hizo, ameahidi kuzifuatilia ikiwa ni mkakati wa
kukabiliana na biashara hiyo.
“Nitazifuatilia hizo kesi kwa kumshirikisha waziri mwenzangu (Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi), ili tujue hizo kesi zimefikia wapi na pia je,
tule (ile) tumifuko (mifuko) twa (ya) dawa za kulevya zimewekwa wapi?
Tusije tukakuta kuna mchanga ndani yake,” alisema Dk. Mwakyembe.
Kuhusu baadhi ya vigogo kudaiwa kujihusisha na biashara hiyo, alisema
kama yupo mtu ambaye anawafahamu kwa majina vigogo hao ampelekee taarifa
kwani suala hili lilipofikia sasa halihitaji usiri.
Dk. Mwakyembe alisema wizara yake itawasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa ili balozi za Tanzania zilizopo nje, zianze
kubana watu wanaojihusisha na biashara hiyo.
Kuhusu maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),
waliodaiwa kula njama za kusafirisha dawa za kulevya kilo 150
zilizokamatwa nchini Afrika Kusini, alisema atashangaa iwapo atasikia
kuwa wamepeleleza na ushahidi haujajitosheleza.
Alisema baada ya kuweka udhibiti katika viwanja vya ndege ambavyo
vinatumiwa kuingiza na kusafirisha dawa za kulevya nchini, hatua
inayofuata ni kubaini wanaowatuma watu wanaokamatwa wakisafirisha dawa
hizo.
Alisema baada ya kuweka udhibiti katika viwanja vya ndege ambavyo
vinatumiwa kuingiza na kusafirisha dawa za kulevya hapa nchini, hatua
inayofuata ni kufanya utafiti watu wanaokamatwa wakisafirisha dawa hizo
ni nani anayewatuma.
Dk. Mwakyembe alisema biashara hiyo itaweza kukoma tu iwapo mipaka yote itadhibitiwa kwa ushirikiano wa vyombo vya dola.
Agosti 15 mwaka huu, Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama wanne
wanaodaiwa kuhusika katika njama za kusafirishwa kwa dawa za kulevya
kutaka wafukuzwe kazi na kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya Sheria
ya Kuzuia Dawa za Kulevya.
Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama hao watakaofukuzwa kazi na
kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya
kuwa ni Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed
Kalungwana.
Mbali na maofisa hao, pia aliliagiza Jeshi la Polisi kumwondoa mara moja
katika uwanja huo, askari wake, Koplo Ernest na kumchukulia hatua za
kinidhamu kwa kushiriki kwake kwenye njama za kupitisha mabegi sita ya
dawa za kulevya, yaliyokamatwa nchini Afrika Kusini.
Pia alisema polisi inapaswa kumsaka Nassoro Said Mangunga aliyevikwepa
vyombo vya dola nchini Afrika Kusini na kutoroka na mabegi matatu ya
dawa hizo.
Dk. Mwakyembe alisema mbeba mizigo katika uwanja huo, Zahoro Mohamed
Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ili
kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai.
Pia ameiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa
maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kuwafikisha kwa
mbwa wakati mwafaka kukagua mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya
na hivyo kuliletea Taifa fedheha kubwa.
Alisema ameamua kuchukua hatua hizo kwa kuwa tukio hilo siyo la kwanza,
bali ni sehemu ya matukio mengi ya upitishaji wa dawa hizo katika uwanja
wa JNIA, ambayo taarifa zake zinaifikia serikali pale watuhumiwa
wanapokamatwa nje ya nchi wakitokea Tanzania.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: