MVUA ILIYOAMBATANA NA UPEPO MKALI DSM HUENDA IKAENDELEA HADI JUMATANO
Mvua iliyoambatana na upepo mkali uliovuma usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam umesababisha umeme kukatika kwa zaidi ya saa sita katika sehemu kubwa ya jiji hilo,miti kuanguka pamoja na wavuvi kusitisha shughuli za uvuvi ili kunusuru maisha yao huku mamlaka ya hali ya hewa ikisema upepo kama huo huenda ukaendelea kutokea nchini hadi Jumatano ijayo.
ITV imepita katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es salaam majira ya asubuhi na kushuhudia miti ikiwa imeanguka pembezoni mwa barabara pamoja na nguzo za umeme zikiwa katika hali ya kutaka kudondoka .
Katika sehemu kubwa ya jiji la Dar es Salaam umeme ulikatika wakati upepo huo ukivuma ambapo mafundi wa shirika la umeme Tanzania -Tanesco wameonekana majira hayo ya asubuhi wakiwa katika harakati za kurejesha umeme.
Nao baadhi ya wavuvi waliokuwa baharini wakivua wakati upepo huo ukivuma wamesema waliamua kusitisha shughuli zao na kuzielekeza mashua na boti walizokuwa wakizitumia katika sehemu zilizo salama ili kunusuru maisha yao.
Kwa upande wao mamlaka ya hali ya hewa kupitia mkurugenzi wake mkuu Agness Kijazi amesema upepo huo umesababishwa na mgandamizo mdogo wa hewa uliopo katika eneo la kusini/magharibi mwa Madagascar ambapo sasa wanalazimika kupata hewa kutoka misitu ya nchi ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo,na hivyo kusababisha upepo mkali unaoambatana na unyevunyevu katika sehemu ambazo hewa hiyo inapita na kwamba hali hiyo huenda ikaendelea mpaka Jumatano ijayo. ITV
0 comments: