SWALI LA MSINGI: NANI HASA NI WAASISI WA MAPINDUZI?


Kwenye historia ya Mapinduzi tufundishwayo shuleni, hayati Sheikh Abeid Amani Karume ndiye anayekua mioyoni mwetu kama muasisi na kinara wa Mapinduzi yaliyofanyika Zanzibar tarehe 12 Januari 1964. Pamoja naye, Abdulrahman Babu, Thabit Kombo Jecha, Abdallah Kassim Hanga na wengineo pia wanajulikana kama waasisi wa Mapinduzi.

Lakini hata hivyo, tunavyoendelea kukua na kudadisi zaidi haswa tukisikiliza stori za wazee wetu waliokuwepo wakati wa Mapinduzi, tunasikia majina mengine ambayo hayatajwi sana kwenye mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Kisultani uliodumu kwa miaka 133 visiwani Zanzibar. Jina kama John Okello ni miongoni mwa majina ambayo yamesahaulika katika kuyapa sifa.

Katika stori hizo, tunaambiwa kwamba viongozi waandamizi wa ASP na vyama vingine, hawakuwepo Zanzibar usiku wa Mapinduzi. Pia, tunaambiwa kwamba, Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa ni 'muoga' wa vita kiasi cha kukimbia Zanzibar wakati Mapinduzi yakifanyika. Inasemekana kwamba, Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika kwa nguvu ya vikundi vidogo vidogo mbali mbali ambavyo havikuwa na mpango mmoja. Vikundi vyote vilitumia advantage hiyo baada ya vijana wa Okello wakiongozwa naye, kuteka kituo cha Polisi cha Ziwani na kuchukua silaha za rashasha.

Wakati haya yote yakitendeka, Karume alikuwa Dar-es-salaam huku vijana wengine wasio wa ASP wakishughulika na Mapinduzi. Tunaendela kuambiwa kuwa, baada ya Mapinduzi kufanyika, Okello ndiye aliyemuamuru Karume kurudi Zanzibar na kumpa urais. Najiuliza maswali mengi kuhusu stori hizi.

Je, ni kweli kwamba hayati Sheikh Abeid Amani Karume ndiye muasisi wa Mapinduzi Zanzibar? Je, stori nzima ya mapambano yaliyodumu kwa saa tisa ya John Okello na vijana wake 200 ni propaganda? Nani aliyefyatua risasi ya kwanza kuashiria kuanza kwa mapinduzi? Nani aliyesimama kidete mstari wa mbele kupigania haki ya Wazanzibari dhidi ya utawala wa Sultan Jamsheed? Je, Okello alikuwa na nguvu gani hadi kumuamuru Karume kurudi Zanzibar? Hayo yote yanabaki kuwa ni maswali ambayo majibu yake yote yapo kwa wazee wetu waliohusika moja kwa moja na Mapinduzi.

Sasa, wazee wanaondoka, nini ambacho vijana tunakibeba kutoka kwao kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar ilhali shuleni tunafundishwa tofauti na stori wanazotupa? Nakaribisha maoni yenu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: