MIAKA MITATU BUNGENI LISU: NILISHA- PIGWA NA KULALA SELO MARA 3



MBUNGE wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uwakilishi wake bungeni, ameshapigwa na polisi kisha kuwekwa mahabusu mara tatu katika maeneo tofauti nchini kwa sababu ya harakati za kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa Global Publishers katika chumba cha habari Bamaga, Mwenge jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii, Lissu alisema kujiingiza katika siasa, hasa katika nchi ambayo haipo tayari kwa siasa za upinzani kama Tanzania, unapaswa kujitoa na kuwa tayari kwa lolote.

“Mimi nina familia yangu, unadhani wanangu wanapenda kumuona baba yao anaadhirika kwa kuchaniwa shati lake na kubebwa msobe msobe? Unadhani mke wangu anapenda kuniona ninadhalilika kwa kupigwa na askari polisi hadharani? Ila nimejitoa na nipo tayari kuhakikisha mambo yanakwenda sawa, hizi ndizo faida za kuwa mwanasiasa wa nchi hii,” alisema.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema ‘mtiti’ wa kwanza kukutana nao ilikuwa ni wakati wa vurugu za wananchi wa wilaya ya Tarime wakati wa mgogoro wao na wawekezaji wa North Mara, mkoani Mara, uliosababishwa na kuuawa kwa watu watatu na walinzi wa mgodi huo.

Lissu alitoa maelezo hayo baada ya kutakiwa kutoa historia ya harakati zake kwa kifupi na kama kuna usawa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Alisema wanasiasa wa upinzani wanachukuliwa kama maadui na ndiyo sababu kila mara wamekuwa wakiwekewa vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao tofauti na wale wa CCM.

“Inataka uthubutu mkubwa kufanya harakati ambazo tunazifanya. Linapokuja suala la kuwatetea wananchi na rasilimali za nchi, inabidi uachane na maono ya kujiangalia kibinafsi, badala yako utazame wajibu wako kama mtetezi wa taifa,” alisema na kuongeza:

“Sidhani kama ni sahihi kuliacha suala la utetezi wa nchi yangu kwa watu wengine. Pamoja na yote ninayofanya bado natembea barabani bila woga, maana ukiogopa kufanyiwa kitu kwa sababu ya harakati, hutaweza kutembea wala kufanya chochote, kwa hiyo siogopi.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: