LITA 29 ZA TINDIKALI ZAKAMATWA HUKO ZANZIBAR.... AL-SHABAB WAHUSISHWA..!!
SIKU chache baada ya Padri wa Kanisa
Katoliki, Parokia ya Machui, Anselm Mwang’amba kumwagiwa tindikali
Zanzibar, Polisi visiwani hapa imekamata lita 29 za tindikali kwenye
magaloni ya ujazo tofauti.
Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi
wa habari katika makao makuu ya Jeshi hilo, Kilimani mjini hapa.
“Jeshi la Polisi limekamata watu 15
kwa matukio mbalimbali...wapo tunaowahoji kuhusu mtandao wa kundi la
Al-Shabaab, lakini wapo wanaohusishwa na matukio ya tindikali, hawa
tunataka kujua wameipata wapi na nani amewauzia,” alisema.
Akizungumzia tukio la mwishoni mwa wiki
la Padri Mwang’amba kumwagiwa tindikali alisema:“Hivi sasa tunazungumza
tukio la kumwagiwa tindikali Padri Mwang’amba Mlandege …upelelezi
unaendelea na watu kadhaa tumewakamata ingawa ni mapema mno kutaja
majina yao, lakini wakati ukifika tutawafikisha mahakamani.”
Akifafanua, Kamanda Mussa alisema Polisi
inakabiliwa na changamoto kubwa ya vitendo vya hujuma kwa kutumia
tindikali dhidi ya watu mbalimbali Zanzibar.
Kuhusu matukio mawili ya kumwagiwa
tindikali kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, Rashid Ali Juma na
Katibu wa Mufti, Shekhe Fadhil Soraga, alisema upelelezi wa shauri hilo
umekamilika na jalada lipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka na Makosa ya
Jinai (DPP).
Shekhe Soraga alimwagiwa tindikali
mwishoni mwa mwaka jana akiwa eneo la Magogoni Msumbiji, Mkoa wa Mjini
Magharibi, wakati akiwa mazoezini.
Wakati akifanya mazoezi hayo, kwa mujibu
wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Yusuf Ilembo, Shekhe
Soraga alimwona mtu mwingine akifanya mazoezi mbele yake kabla ya
kumgeukia na kummwagia tindikali iliyomjeruhi usoni na kifuani.
Baadaye mtu aliyefanya unyama huo,
alitoweka na kuelekea kusikojulikana. Mbali na Shekhe Soraga, mwanzoni
mwa Agosti, walimu wawili wa kujitolea raia wa Uingereza, Kate Gee (18)
na Krisdtie Trup (18), walijeruhiwa kwa tindikali, wakati wakienda kula
usiku.
Akizungumzia upelelezi wa tukio hilo,
Kamanda Mussa alisema upelelezi uko hatua za mwisho kukamilika. Kutokana
na uhalifu huo, walimu hao walikimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan
Dar es Salaam kupewa huduma na baadaye walirudishwa kwao kwa matibabu
zaidi, na mmoja wao anatarajiwa kupandikizwa ngozi.
Msako
Kuongezeka kwa matukio hayo,
kumesababisha Polisi Zanzibar kuanza operesheni kwa kushirikiana na
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa lengo la kupunguza matumizi holela
ya tindikali.
Kamanda Mussa alisema operesheni hiyo ilianza Jumamosi na inalenga waagizaji, wasambazaji na watumiaji wa tindikali kwa ujumla.
Kwa usimamizi wake, Kamanda Mussa
alisema msako maalumu umeanza katika maduka yanayouza tindikali ili
kujua kama wanamiliki vibali halali vya biashara hiyo.
“Msako wa tindikali umeanza na sasa
tumeanza ukaguzi wa maduka ya biashara hiyo kujua kama wana leseni ya
kuiendesha,” alisema. Pia Polisi imeanza kukutana na wadau kuangalia
sheria ya kumiliki tindikali na matumizi yake ikiwamo kudhibiti tatizo
hilo.
Al-Shabaab
Kati ya watuhumiwa 15 wa kikundi cha
kigaidi cha al Shabaab wanaoshikiliwa Polisi, Kamanda Mussa alisema
baadhi yao ambao hakuwataja majina, wanatuhumiwa kuhusika na kikundi
hicho na itikadi za imani kali za kidini.
Al-Shabaab, yenye asili yake Somalia,
ina lengo la kutafsiri Sheria za Kiislamu katika namna ya imani kali ya
kidini. Kikundi hicho kinadaiwa kupewa mahitaji ya kifedha kutoka
vikundi vya kimataifa vya kigaidi, baadhi ya nchi na wananchi wa Somalia
wanaoishi nje ya nchi yao.
Wanazuoni
Taarifa ya wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania (Hay-atul Ulamaa), iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari,
ilitaka Watanzania kurejea kwenye utamaduni wa karne nyingi zilizopita,
wa kuvumiliana na kushirikiana kulinda amani nchini.
Mwenyekiti wa wanazuoni hao nchini,
Shekhe Sulaiman Kilemile, alieleza katika taarifa hiyo, kwamba kitendo
cha Padri Mwang`amba kumwagiwa tindikali, hakikubaliki na ni wajibu wao
kukilaani kwa nguvu zote.
“Hivi ni vitendo vinavyoashiria chuki
baina ya Watanzania wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vikiachwa viendelee
vitasababisha amani, utulivu na busara kutoweka nchini,” alieleza Shekhe
Kilemile katika taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia ilikemea matumizi ya
silaha za moto kama ilivyotumika kumwua Padri Evarist Mushi, na
kumjeruhi Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Ponda Issa
Ponda.
“Matukio kama hayo yote ni hatari ambayo
yanaweza kubadili sura nzuri ya Tanzania…tunachukua nafasi
kuwahadharisha viongozi wa dini na wengineo wasikurupuke kuelekeza
tuhuma kwa kikundi kimoja dhidi ya kingine. “Hivyo si halali tukio kama
hilo kuhusishwa na udini, uzanzibari na utanganyika kabla ya kufanya
uchunguzi na kupata dalili sahihi za kutosheleza,” alisema Shekhe
Kilemile.
Askofu Shao
Katika hatua nyingine, Askofu wa Kanisa
Katoliki, Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao, amesema usalama wa viongozi
wa dini umekuwa mdogo Zanzibar kutokana na kuendelea kupokea vitisho.
Askofu Shao alisema hayo Dar es Salaam,
alipokwenda kumjulia hali Padri Mwang’amba, ambaye amelazwa Muhimbili.
Padri Mwang’amba alisema Julai alipokea vitisho kutoka kwa vijana ambao
hufanya mazoezi katika njia ambayo yeye hupita kwenda kuona wazee,
lakini hana uhakika kama ni vijana hao ndio wameshiriki uhalifu huo.
“Siwezi kusema moja kwa moja kama ni hao
vijana, maana walinitolea vitisho kuwa ipo siku watanifanyia kitu
kibaya kwa kuwa nawasumbua wakati wanafanya mazoezi. “Siwezi kusema moja
kwa moja kuwa ni wao ama ni mwendelezo wa matukio ya watu wanaofanya
uhalifu kwa kuwamwagia wenzao tindikali,” alisema Padri Mwang’amba.
Aliongeza kuwa baada ya kupokea vitisho
hivyo alitoa taarifa Polisi na hali ikaendelea kuwa shwari, kwani
hakupokea tena vitisho mpaka alipomwagiwa tindikali.
Aliziomba mamlaka husika kuhakikisha
wahusika wanatafutwa na kuchukuliwa hatua, pia kudhibiti matukio ya aina
hiyo ambayo yamekuwa yakijitokeza visiwani humo.
Askofu Shao alisema vitisho wanavyopata
ni vingi zaidi, pia hawawezi kujua madhumuni na makusudi ya matukio
hayo, kutokana na kuwepo kwa migongano tofauti ya kisiasa, kidini na
mingineyo.
Alisema asilimia kubwa ya matukio
yanayotokea yamekuwa yakilenga dini moja na kufanya viongozi wa dini
kuhofia usalama wao. “Kwa tukio hili hii ni ishara tosha kwamba usalama
wetu ni mdogo sana, sasa hivi tunaogopa hata kutembea,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments: