JWTZ LAKAMATA WANAJESHI WANNE WA RWANDA WALIOKUWA KONGO WAKIWASAIDIA WAASI WA M23..


ASKARI wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani nchini Kongo (Monusco), wakiongozwa na vikosi vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wamedai kuwakamata maofisa wanne wa jeshi la Rwanda, katika mapigano ya wiki iliyopita nchini Kongo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa askari aliyepo ndani ya kikosi cha JWTZ huko nchini Kongo, alisema maofisa hao wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Taarifa hizi za sasa zinakuja wakati ambapo kumekuwa na madai ya muda mrefu, ambayo yamekuwa yakitolewa na Umoja wa Mataifa pamoja na Marekani kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia waasi wa kundi la M-23.

Pamoja na kwamba Rwanda imekuwa ikipinga madai hayo, kitendo chake cha wiki iliyopita cha kuamua kupeleka bataliani mbili zenye wanajeshi 1,700 ili kukabiliana na kile kinachodaiwa kuwa ni kishindo cha vikosi vya Umoja wa Mataifa vyenye jukumu la kulinda amani katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa kirasilimali, kinatokana na waasi wa M23 kupata kipigo kikali.

Chanzo chetu hicho kutoka uwanja wa mapambano nchini Kongo, kililidokeza gazeti hili kuwa maofisa hao wa Jeshi la Rwanda waliwakamata katika mapigano hayo yaliyodumu kwa zaidi ya wiki moja, ambayo tayari yamewakimbiza waasi wa M23.

“Askari wa Rwanda tuliowakamata, ni maofisa wa ngazi za juu kabisa jeshini, tena walikuwa na sare za jeshi hilo… walikuwa wakiwasaidia hao M23, lakini kwa kuwa sisi tulikuwa makini tulifanikiwa kuwatandika hadi tukawakamata,” kilisema chanzo chetu hicho.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vya habari vya kuaminika zinaeleza kwamba, hatua hiyo ya kuwakamata maofisa hao pamoja na kuondoka kwa waasi wa kikundi cha M23, imefanikisha kushinda vita hiyo kwa zaidi ya asilimia 95.

Mtoa taarifa wetu huyo kutoka Kongo, ameliambia gazeti hili kuwa, tayari Monusco wanaoongozwa na JWTZ wameanza kufurahia ushindi huo na kwamba sasa hivi wanasubiri tamko kutoka kwa wakuu wao, ili kufahamu kinachofuata baada ya kufanikisha hatua hiyo.

MAPIGANO YALIVYOKUWA

Akielezea namna walivyofanikiwa kutoa kibano kwa M23, askari huyo kwanza alikiri kuwa mapigano yalikuwa makali, kutokana na kikundi hicho cha waasi kusheheni vifaa vya kisasa na msaada wanaoupata kutoka Serikali ya Rwanda.

“Kwa kweli mapigano yalikuwa makali sana, lakini kwa upande wetu sisi tulikuwa tunajiamini kutokana na vifaa ambavyo pia ni vya kisasa hususani ikizingatiwa jeshi letu ni la Umoja wa Mataifa.

“Tulifanikiwa kuteka ngome yao kwa kutumia mbinu mbalimbali za kijeshi na kuwafanya watawanyike kabisa katika eneo hilo.

“Ngome yao ilikuwa ni kubwa sana, ina ukubwa wa zaidi ya viwanja vitatu vya mpira… na katika eneo hilo kulikuwa kumesheheni vifaa vyao vya kivita, kama makombora, mafuta, mizinga pamoja na vifaa vingine kama magari na baadhi ya silaha nyingine kubwa kubwa za kivita,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, sasa hali ni shwari ndani ya nchi hiyo ya Kongo.

“Baada ya kuwasambaratisha sasa wamekimbilia eneo moja lililopo karibu na mpaka wa Uganda. Kama unavyofahamu hawa jamaa walikuwa wakitumia mbinu za kujihami kwa kurusha mabomu katika eneo la Rwanda, ili ionekane kuwa sisi tumerusha,” alisema askari huyo.

“Lakini tunamshukuru Mungu, tupo salama ingawa tumempoteza askari mmoja na askari wengine wenzetu wa Tanzania ambao ni wanne, wamepata majeraha kidogo lakini wanaendelea vizuri.

“Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu waendelee kutuombea turudi salama, kwa sababu kazi sasa imeshakamilika,” alisema askari huyo.

Juhudi za gazeti hili kumpata msemaji wa Monusco, Luteni Kanali Prosper Basse kuzungumzia juu ya taarifa hizo, zilishindikana.

Taarifa ambazo tumezinasa kwa siku kadhaa sasa kutoka uwanja wa mapambano na ambazo zimegusa vichwa kadhaa vya habari zinaeleza kuwa, brigedia maalumu ya vikosi vya UN yenye dhamana ya kujibu mashambulizi (FIB), katikati ya wiki iliyopita iliendesha operesheni kubwa iliyoharibu kabisa ngome muhimu ya waasi wa M23, hali inayotajwa na wachambuzi wa mambo kuwa ndiyo iliyoishtua Serikali ya Rwanda ambayo inatuhumiwa kuwasaidia waasi hao.

Taarifa za kijeshi zinaeleza kuwa, FIB ambayo inaundwa na wanajeshi wapatao 3,000 kutoka Tanzania na Afrika Kusini chini ya Azimio Namba 2098 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limejizatiti kwa zana za kisasa za kivita zikiwamo mizinga na helikopta za kivita.

Taarifa kutoka mashariki ya Kongo zinaeleza kwamba, mashambulizi dhidi ya waasi wa M23 ambao hivi karibuni waliripotiwa kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Tanzania aliye katika jeshi la UN, yamesababisha waasi hao kukimbilia katika eneo la milima lililopo umbali wa kilomita tano kutoka mji mdogo wa Kanyaruchinya Mashariki mwa Goma.

M23 WAZUNGUMZA

MTANZANIA Jumatano jana lilifanikiwa kuzungumza na Rais wa M23, Bertrand Bisiimwa, ambapo pamoja na mambo mengine alieleza sababu za vikosi vyao kuondoka katika ngome yao ya kivita sambamba na taarifa za kuibuka kwa mapigano mapya ya hivi karibuni.

Katika hilo, Bisiimwa alikiri kikosi chake kurudi nyuma siku nne zilizopita, huku akiitaja sababu ya kufanya hivyo kuwa ilitokana na wao kutotaka vita baada ya majeshi ya Kongo kuanza kuwarushia mabomu kwenye kambi yao.

“Sisi tuliamua kurudi nyuma tusiendeshe vita, tunajua aliyetupa hayo mabomu ambayo yalifika mpaka Rwanda, tunaitaka Umoja ya Mataifa ikuje ifanye uchunguzi wake…wakuje waangalie vifaa yetu waone kama inaweza kurusha mabomu hadi Rwanda,” alisema.

Hata hivyo, Bisiimwa alisema kuwa sio kweli kama majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiongozwa na JWTZ yaliwasambaratisha katika ngome yao.

“Sio kweli walikuja Kanyaruchina tukiwa tumeondoka na tuliondoka si kwa sababu ya kuwakimbia, hapana tulitaka UN wafanye uchunguzi yake juu ya kurushwa mabomu, kwa sababu wanataka kutuvalisha mambo ya uongo mchafu,” alisema Bisiimwa.

Bisiimwa alijigamba kuwa majeshi ya Kongo hayawawezi na kwamba walikwishawashindwa, lakini akakiri kwamba majeshi ya Umoja wa Mataifa wanaweza kuwaondoa.

“Ninakiri hiyo kwa sababu Umoja wa Mataifa inaweza kututoa, unajua inakuwa na nguvu ya hatari,” alisema Bisiimwa kwa Kiswahili cha tabu.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: