MKE WA MTU ANUSURIKA KUUAWA BAADA YA KUNASWA AKIIBA NGUO KARIAKOO


Jimama mwenye hadhi yake ambaye ni mke wa mtu aliyetajwa kwa jina moja la Mary au Mama Gilo, mkazi wa Sinza jijini Dar amekula kichapo cha kutisha almanusra apoteze uhai baada ya kunaswa akiiba nguo kwa ajili ya Sikukuu ya Eid El Fitr.



Tukio hilo la aibu lililoshuhudiwa na  mwandishi wetu lilijiri katika moja ya maduka makubwa ya nguo Kariakoo, Dar mwishoni mwa wiki iliyopita.


Mama Gilo ambaye anafahamika Kariakoo na Sinza, alinaswa akiiba nguo za sikukuu ikiwa ni pamoja na ‘madira’ ya kumalizia mfungo.



Katika tukio hilo lililokusanya kadamnasi, mwanamke huyo alipigwa chabo kwenye duka la mfanyabiashara Rehema Kessy ambapo alidai kuwa alifika Kariakoo kwa lengo la kununua madira lakini alijikuta akiingiwa na tamaa ya kuiba ndipo akanaswa.


Awali, kabla ya kuwekwa chini ya ulinzi na raia waliokuwa na hasira kali, mwanamke huyo alidaiwa kukwapua mkoba wa mwanamke mwenzake na kujichomeka kwenye maduka kumkwepa aliyemuibia ‘pimajoto’ lake linalodaiwa kuwa na vitu ndani yake.


Baada ya kutiwa mikononi ndipo watu waliokusanyika wakauliza: “Na tumfanye nini mwanamke huyu?”
Watu wakapaza sauti wakisema: “Kwa utaratibu wetu hapa Kariakoo kwa mwizi yeyote, hakuna adhabu nyingine zaidi ya kusulubiwa hadharani.”


Ndipo ikaamriwa asulubiwe kwa kupewa bonge la kipigo na kufanya watu kutanda kwenye duka hilo kwa muda wa saa nzima bila kutoka, wakitaka aachiwe ili wamalize kazi yao ya kumtoa roho kama adhabu ya mwizi anapokamatwa Kariakoo.


Katika kusulubiwa huko, Mary alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa akisema: “Naombeni mnisamehe, nimekuwa nanyi siku zote tukifanya biashara ya madira, leo mnaniua? Naombeni mumpigie simu mume wangu baba Gilo aje anisaidie.”
  

Alipoambiwa akiri kuhusika na upotevu wa madira madukani katika mazingira ya kutatanisha kisha atasamehewa, alisema: “Ni kweli nakiri mbele yenu na Mungu awe shahidi, nimekuwa nikifanya kazi hii (kuiba madira) pamoja na wanawake wenzangu watatu lakini wamenikimbia.”


Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, si mara ya kwanza kwa Mary kukamatwa kwa wizi kwani mwanzo aliwahi kudakwa, akavuliwa mpaka nguo lakini amerudia tena kazi hiyo.


Ili kumnusuru, mmoja wa wasamaria wema aliyehisi uchungu kwa kuwa mwanamke huyo alikuwa akilalamika kuwa anakata roho, aliwapigia simu polisi wa Kituo cha Msimbazi, Kariakoo na kuwaambia: “Wahini mara moja hapa jirani na shimoni. Kuna mwanamke mwenye hatia ya wizi anasulubiwa. Njooni mumuokoe.”


Ndani ya ‘dakika sifuri’ polisi na ulinzi shirikishi walifika eneo la tukio lakini walipomuona mtu waliyekuja kumuokoa akiwa ameshalegezwa ,  ikabidi waagize tolori la kumbebea.


Tolori liliposogezwa jirani na mwanamke huyo alipakizwa na kumkimbiza huku wananchi wakimsindikiza kwa kumzomea wakati wengine wakitaka kumponda na mawe hadi afe.


Mwisho wa yote mwanamke huyo alikwenda kubwaga kituoni Msimbazi akiwa amepoteza fahamu kisha kufanyiwa utaratibu wa  matibabu kabla ya kesi .

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: