BAADA YA DOGO JANJA KUOMBA MSAMAHA ILI ARUDI TIP TOP, HII NDIYO KAULI YA MADEE NA BABU TALE VIONGOZI WA TIP TOP
Dogo Janja kuuomba msamaha kupitia vyombo vya habari uongozi wa Tip Top Connection na Madee aliyemtoa Arusha, Boss wa Tip Top Connection Babu Tale ameiambia tovuti ya Times Fm kuwa anataka rapper huyo aseme ukweli wa yote aliyoyasema awali baada ya kutoka Tip Top.
“Aongee ukweli tu haina shida, nimemsamehe yeye ni Muislamu mwenzangu tumetumwa tusameheane, mimi nimeshamsamehe ila nimezungukwa na mashabiki ambao wakati yeye ananitukana kuna mashabiki ambao walikuwa upande wangu ingawa walikuwa hawajui kama dogo alikuwa anaongea ukweli au uongo.” Amesema Babu Tale.
“Babu Tale ameweka wazi vipengele ambavyo anataka Dogo Janja aviweke sawa.
“Dogo anatakiwa aseme kama kweli aliibiwa, kama kweli alidhurumiwa na kama kweli hajawahi kuishi nyumbani kwa Madee. Anatakiwa aongee dhahiri asifiche, aongee tu ukweli.” Babu Tale ameeleza.
Amegusia pia tukio ambalo lilimsikitisha zaidi wakati Dogo Janja anafanya kazi akiwa chini ya menejimenti ya Mtanashati Entertainment.
“Siku zote kwenye ukweli uongo hujitenga, wakati yuko South Africa alipost picha ‘ningekuwa Tip Top nisingefika huku’. Nilishangaa heeh huyu kutoka huko kijijini kwao alifanyaje hadi kufika hapa!
“Wazazi wake nao wakawa wamekubali uongo wa mtoto wao wakaanza kutuongelea na sisi maneno ambayo ni uongo. Ulikuwa uongo wa watoto halafu bado wao wanakandamiza uongo zaidi ya uongo. Kwa kuwa ni mtoto kuna wazazi ambao walisimama nyuma yake ambao nao walikuwa wanasapoti. Aongee ukweli mimi ntamsaidia.” Babu Tale ameeleza.
Babu Tale ameeleza kuwa Dogo Janja ameshamtafuta kwa njia ya simu lakini amemwambia ujumbe ule ule kuwa awaambie ukweli watanzania.
Kwa upande wa dogo janja, ameongea na Tovuti ya Times Fm na hakutaka kuizungumzia kwa undani kauli ya Babu Tale, zaidi alieleza kuwa alichokifanya kuomba msamaha alimaanisha kuwa alikuwa amekosea na hakuna aliyemsukuma kufanya hivyo.
Ameeleza kuwa endapo atakaribishwa tena Tip Top Connection atajiunga na kundi hilo japo ameeleza kuwa kuomba kwake msamaha hakuwa na maana kuwa alikuwa na lengo la kurudi Tip Top.
“Mimi nimeomba msamaha kwa kuwa nataka kuweka mambo sawa na kumaliza tofauti na uongozi wangu wa zamani. Hivyo tu. Wakinikaribisha Tip Top itakuwa poa tu pia…fresh.”
Times Fm ilimtafuta Madee ambaye alisema kuwa bado hajawa tayari kuongelea suala hilo na kwamba mtu anaeweza kuzungumzia suala hilo kwa sasa ni Babu Tale.
0 comments: