WATOTO WALIO ZALIWA WAMEUNGANA WAREJEA DAR BAADA YA KUTENGENISHWA


Watoto pacha, Elikana na Eliud waliokuwa wameungana wamerejea nchini jana wakitokea India walipokuwa kwa ajili ya kutenganishwa, tayari kwa kusherehekea kumbukumbu yao ya kutimiza mwaka mmoja leo.

Waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere saa 10:30 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Oman, wakiwa na mama yao, Grace Joel (20) ambaye muda wote alionekana mwenye furaha.

Elikana na Eliud walizaliwa Februari 20, mwaka jana wilayani Kyela, Mbeya wakiwa wameungana na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya ambako walipata rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Juni mwaka jana, Serikali iliwapeleka Hospitali ya Chennai, India ambako Desemba 16, mwaka jana walifanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha.

Akizungumza baada ya kutua jana, Grace alisema: “Nina furaha ya ajabu, sijui nimshukuru vipi huyu Mungu wangu, ni mkuu mno. Ninawashukuru sana madaktari wa India, ninawashukuru madaktari wa Muhimbili na sana naishukuru Serikali yangu kwa kunipa msaada huu mkubwa. Siamini kama leo ningekuwa narudi salama na watoto wangu kila mmoja akijitegemea,” alisema Grace.

“Kesho (leo) ni birthday yao, wanatimiza mwaka mmoja, ni furaha ya ajabu niliyo nayo, siwezi kuelezea. Siku nilipoambiwa watoto wangu watafanyiwa upasuaji mkubwa na watapumulia mashine kwa wiki moja, nilichanganyikiwa kwa kweli, sikutamani tena hata hiyo operesheni ifanyike ila sikuwa na jinsi zaidi ya kumwomba Mungu.”

Akizungumza uwanjani hapo, Dk Glory Joseph kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando ambaye aliongozana na watoto hao kurudi nchini alisema: “Watoto wamerejea salama na wanaendelea vizuri ila watakuwa Moi (Hospitali ya Mifupa Muhimbili), kwa uangalizi maalumu mpaka hapo madaktari watakapoona inafaa ndipo watapewa ruhusu ya kurudi nyumbani kwao Mbeya.

“Agosti watarudishwa tena India kwa ajili ya upasuaji katika njia ya mkojo na kufunga sehemu ya utumbo,” alisema.

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alisema upasuaji wa watoto hao ulichukua saa 18. Katika muda huo, saa 13 zilitumika kutenganisha viungo vilivyoungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo, sehemu ya utumbo mpana, njia ya mkojo, kibofu na sehemu ya uume, wakati saa tano zilitumika kuunganisha sehemu zilizotenganishwa.

Pacha hao walifanyiwa upasuaji na madaktari 20 na wataalamu wengine wa afya ambao walitumia saa 18 kuwatenganisha. Kiasi cha Sh100 milioni kilitumika.

Meneja wa Huduma za Wagonjwa wa Kimataifa wa hospitali hiyo, Senu Sam alizungumza na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen juzi na kusema wamefanya sherehe kwa ajili ya mafanikio ya upasuaji huo.

Sam alisema pacha hao wameonana ana kwa ana kwa mara ya kwanza, wiki tatu baada ya upasuaji... “Imekuwa faraja kuwaona wakitazamana. Eliudi alivishika vidole vya mkono wa Elikana na kuvichezea. Wanaonekana kufurahia mazingira mapya,” alisema Sam.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: