HIVI NDIVYO VYAMA VYA UPINZANI VILIVYONGURUMA JANA..MSWADA WA KATIBA WAPIGWA VIKALI



Vyama vya upinzani jana vilifanya mkutano mkubwa kuwashawishi wananchi kupinga kile walichokiita kuhujumiwa kwa mchakato wa Katiba Mpya, wakitangaza Oktoba 10 kuwa siku ya Watanzania wote kushiriki katika maandamano kushinikiza wapewe haki ya kuandaa Katiba yao.

Wakizungumza kwa kupokezana katika Viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam jana, wenyeviti wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, walieleza kuwa wataendelea kushirikisha taasisi za kiraia kupinga hujuma dhidi ya mchakato wa Katiba Mpya na kwamba hawatakubali endapo Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.

Akizungmza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema chama chake hakitakubali endapo Rais Kikwete atasaini muswada huo kwa kuwa una lengo la kupata Katiba Mpya isiyokuwa na tija kwa taifa. Alisema kuwa Katiba inayoandaliwa ni kwa ajili ya Watanzania wote na siyo kundi la watu, hasa CCM na kwamba mchakato wa kuwapata wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka makundi mbalimbali siyo sahihi.

“Haiwezekani kila taasisi ikateuwa wajumbe tisa ambao majina yao yatakwenda kuchakachuliwa na usalama wa taifa, kisha kupata majina ya watu wanaowataka wao, kitu hiki kama CUF hatutakubali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Hatutarudi nyuma na kukubali kuendelea na mchakato huu endapo Rais atasaini muswada huu. Tutaendeleza harakati za kupinga kwani bila hivyo tutapata Katiba Mpya isiyokuwa na tija.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa ni wakati wa kukaa meza moja ya mazungumzo kuondoa tofauti zilizopo ili kulinusuru taifa kuingia katika machafuko.

Alisema kama taifa, linatakiwa kujifunza kutoka mataifa mengine yalivyotokea maafa katika michakato ya kuandikwa kwa Katiba Mpya.

“Ni wakati wa kukaa meza moja, kwa kushirikisha wadau mbalimbali kwani Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote na siyo ya CCM,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Lazima tupate Katiba Mpya kwa gharama yoyote ile, iwe ndani au nje ya Bunge ili kuhakikisha tunapata Katiba ya Watanzania wote.”

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema kosa kubwa katika kudai haki ni woga na hatutapata Katiba Mpya kama tutaendelea kuwa taifa la watu wenye hofu. Tunataka kukutana na makundi mbalimbali katika jamii ambayo ni viongozi wa dini, wasomi na watu wa makundi mengine kuwaeleza kinachoendelea sasa hivi.

Hata migogoro ya kiimani baina ya Wakristo iliyotokea nchini imesababishwa na katiba iliyopo sasa, kama Rais atasaini wao hawatashiriki Bunge la Katiba na watatumia kila mbinu iliyopo duniani kuueleza umma nini kimetokea na hawataendelea kunyenyekea vitisho vya Jeshi la Polisi.

Tunalaani mchakato wa katiba kuhodhiwa na chama kimoja na tunatangaza Oktoba 10, mwaka huu kuwa ni siku maalumu ya kudai katiba na sasa hawataenda tena Ikulu kwani inaaminika huko ni kwenda kunywa chai na watatangaza maandamano nchi nzima.


Tumemwambia IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema) kuwa hatutaomba ruhusa bali tutampa taarifa.Tunaomba walio makanisani na misikitini kutafuta katiba mpya na jambo la mwisho Jumatato tutaenda kufanya mkutano kama huo Zanzibar,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema chama chake kinapinga namna mchakato wa Katiba ulivyoendeshwa kwasababu kilichopelekwa bungeni kilikuwa Muswada wa Katiba Mpya, lakini kilichopo mitaani ni Mchakato wa Rasimu ya Katiba Mpya.

“Tunawaambia CCM hawatengenezi Katiba Mpya, wanachofanya ni danganya toto kwa kuwa wanatakiwa kuirudisha Katiba ile ile ya awali.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe aliyefika katika viwanja hivyo alisema kuwa Rais Kikwete akisaini muswada huo, Watanzania watajua kuwa hana nia njema na taifa kwa kuwa wengi wanaipinga.

“Mimi natega masikio kusikia kama utasaini au la ili kujua kama unawatega na kuwahadaa Watanzania. Tunakuomba usikubali mtego huo,” alisema Kakobe akimwambia Rais Kikwete.

Alisema tangu awali CCM ilikuwa ikipinga kuandaliwa kwa Katiba Mpya, ingawa Rais Jakaya Kiwete alijitosa na kukubali mchakato huo kuanza nchini.

“CCM ilikataa katakata Katiba isianzishwe. Jakaya Kikwete pekee yake alijipiga kifua akakubali ingawa alishambuliwa kuwa amefanya makosa,” alisema Kakobe.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kukuu cha Dar es Salaam(Udsm), Dk Azaveli Lwaitama alisema kuwa duniani kote shinikizo la kuundwa kwa Katiba Mpya hutoka nje ya Bunge na Serikali iliyopo madarakani.

“Tangu mwaka 1992 vyama vya upinzani vilikuwa vikitaka Katiba Mpya... Katiba Mpya huzaliwa na wanamapinduzi waliopo nje ya Bunge,” alisema Dk Lwaitama.

Akizungumzia ushirikiano wa vyama kumzuia Rais asisaini Sheria ya Rasimu ya Katiba, alisema: “ Ukifanya jeuri kwa sababu upo madarakani, watu uliodhani wamegombana watashirikiana.”

Mbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema Mahakama ya wananchi ndiyo itakayotoa uamuzi wa mwisho.

“Ninyi ndiyo Mahakama yenye uamuzi wa mwisho, tunasubiri mwongozo wenu, mtakachosema tutafanya,” alisema Mnyika.

Kabla kuwasili kwa viongozi wakuu wa vyama hivyo vya siasa kwenye Viwanja vya Jangwani, jana wafuasi wao walikuwa kwenye makundi wakichambua baadhi ya mambo yaliyoonekana kuleta utata kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Rangi za bluu, nyekundu na nyeupe zinazotumiwa na vyama vilivyoshiriki kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya zilionekana kuzagaa katika viwanja hivyo.

Magari ya Polisi yalionekana kuzunguka maeneo ya viwanja hivyo kuhakikisha ulinzi unaimarika wakati wote wa mkutano.

Nao wafuasi wa vyama hivyo waliokuwa wamevaa suti nyeusi, miwani na mashati meupe waliimarisha ulinzi katika eneo la mkutano, wengine wakiingia Viwanja vya Jangwani kutoka eneo la Barabara ya Morogoro, huku wakibeba mabango, bendera za vyama hivyo na picha za viongozi wao wakiimba nyimbo mbalimbali.

Wengi wa wafuasi hao walifika uwanjani hapo kwa kuletwa na mabasi madogo aina ya Coaster na wengine wakija kwa makundi kutokana Jeshi la Polisi kuzuia kufanyika kwa maandamano.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: