ANGALIZO:MAFUTA YA UBUYU YANA TINDIKALI INAYOSABABISHA SARATANI


Baada ya kuonya wananchi wanaotumia dawa za tiba mbadala ambazo hazijathibitishwa, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), sasa inawataka wananchi kuacha kutumia mafuta ya ubuyu kwa kunywa kama dawa.

Akizungumza juzi katika Maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema Mamlaka hiyo ilipima na kubaini mafuta hayo yana tindikali ya mafuta.

 

Alifafanua katika maonesho hayo maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, kwamba mafuta hayo hayafai kuliwa na binadamu na anayekunywa kwa wingi, yuko hatarini kupata saratani za aina tofauti tofauti.

"Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la wajasiriamali wanaouza mafuta ya ubuyu kama dawa, kwa kuwaelekeza wananchi kunywa. Napenda kuwataarifu kuwa mafuta hayo ni hatari kwani yana tindikali ya mafuta," alisema.

 

Mwandishi alipata sampuli ya vielelezo vya matumizi yake na manufaa yake mwilini, kama inayotangazwa na wajasiriamali katika maeneo mbalimbali na hata katika mitandao. 

 

"Ni mafuta yatokanayo na mbegu za ubuyu {au kokwa}. Hukamuliwa kiini chake na kutoa mafuta. Yana ubora kuliko mafuta mengine ya kupikia, yana Vitamin A, B, C, D na F. Pia yanatibu magonjwa mbalimbali," kielelezo kimoja kilinadi ubora wake katika mitandao ya jamii.

Mafuta hayo yamedaiwa kutengeneza seli zote ndani ya mwili, kuzuia ngozi isiharibike wala kupata makunyanzi, kuondoa mafuta  ndani ya mishipa ya damu na yanapunguza uzito uliozidi.

 

Pia inadaiwa yanarutubisha ini na figo, yanaleta hamu ya kula, yanaimarisha mifupa, kucha na nywele, yanaongeza kinga ya mwili (CD4), yanaondoa sumu na yanatengeneza sukari iwe katika kiwango kinachotakiwa.

 

Maelezo hayo yameendelea kusifu kwamba yanasaidia kuona vizuri na kujenga kumbukumbu, yanapunguza vitambi na matumbo makubwa, yana virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini.

Katika ngozi yametajwa kuondoa madoa, chunusi, fangasi, upele, mba na muwasho, yanafaa kwa walemavu wa ngozi (albino). Pia huondoa hamu ya kutumia dawa za kulevya na kuponyesha vidonda vya tumbo.

 

"Endelea kutumia mafuta bora ya ubuyu, ni bidhaa asilia ya kitanzania. Ni mafuta yasiyochanganywa na kitu chochote, ni mafuta asilia,"  yamesifiwa katika maelezo hayo.

 

Mtumiaji ameelezwa kama ana ugonjwa wa kisukari, atumie kijiko cha chakula kimoja tu. Anatakiwa kutumia dozi hiyo ya kwanza nusu saa kabla ya kula chochote kwa muda wa siku 15.

 

Dozi ya pili na ya tatu kwa wagonjwa hao, inatakiwa kufuata baada ya siku 15 kisha mgonjwa apumzike wiki moja, huku akiendelea kupima kila wiki. Kipimo hapo ni cha hospitali.

Kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo, figo na ini, wameelekezwa na wajasiriamali hao kunywa kijiko cha chakula kimoja asubuhi kabla ya kula chochote, na usiku kijiko cha chakula kimoja kabla hajala chochote kwa muda wa siku 15 kwa dozi ya kwanza.

 

Baada ya hapo, mgonjwa anapumzika wiki moja kisha siku 15 zinazofuata dozi ya pili, mapumziko wiki moja halafu siku 15 nyingine dozi ya tatu. 

 

Maelezo ya dozi hiyo ya kutibu ugonjwa wa vidonda vya tumbo, yanaendelea kumtaka mgonjwa baada ya dozi ya tatu, aanze kunywa kila wiki mara moja kijiko cha chakula kimoja asubuhi, tena nusu saa kabla hajala chochote kwa muda wa wiki nne.

 

Dozi inaendelea ambapo mgonjwa atatakiwa kunywa kijiko kimoja cha chakula kila mwezi mara moja asubuhi, kabla hajala chochote kwa muda wa wiki nne, kisha kunywa kila mwezi mara moja, asubihi kabla hajala chochote kwa muda wa miezi sita mfululizo.

 

Kwa utoaji wa sumu, mgonjwa ametakiwa kunywa kijiko cha chakula kimoja asubuhi kila siku kwa muda wa siku 14, kisha kunywa kila mwezi mara moja kwa muda wa miezi sita mfululizo.

 

Kwa kuongeza CD4 mwilini, ametakiwa kupata kijiko cha chakula kimoja asubuhi nusu saa kabla ya kula chochote, na usiku kijiko cha chakula kimoja nusu saa kabla ya kula chakula cha usiku kwa muda wa miezi mitatu.

"Mgonjwa aanze kunywa baada ya kipimo cha mwisho (cha CD4) alichopima. Mafuta yanapatikana kuanzia ujazo wa lita moja na zaidi," imesifiwa dawa hiyo.

 

TFDA imeonya kuibuka kwa tabia ya wananchi kutaka matibabu ya haraka, kama ilivyo kwa baadhi ya watu kutaka utajiri wa haraka, na imehadharisha ni vema kabla ya kutumia dawa zinazoibuka kila siku, waulize kama zina ubora kwa afya zao.

 

"Nawasihi wananchi kuacha kukimbilia dawa ngeni mara tu baada ya kutangazwa kama haya Mafuta ya Ubuyu, yamekuwa yakielezwa ni dawa na wajasiriamali tu, na wengi wamekuwa wakitumia bila kusikiliza mamlaka husika zinasemaje," alisisitiza.

 

Semwanza alisema Mamlaka hiyo iko katika mkakati wa kuanza kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya mafuta hayo, ambayo wengi wanayaamini na kuyanywa kama dawa.

 

Kwa mujibu wa Semwanza, baada ya kupima mafuta hayo na kubaini hatari hiyo, waligundua pia inawezekana tindikali hiyo kutenganishwa na mafuta hayo, lakini imebainika utaalamu na teknolojia hiyo haipo nchini.

 

Hata hivyo, alisema Mamlaka hiyo haijabaini madhara ya matumizi mengine ya mafuta hayo kama kipodozi.

 

Kutokana na mvuto huo wa kibiashara, na shauku ya kupona haraka ya wananchi, Semwanza alisema TFDA imekuwa ikifanya msako wa dawa mbalimbali zinaouzwa na wajasiriamali katika maonesho hayo.

 

Alisema kuwa kuna baadhi ya waandaaji wanaowaalika wajasiriamali bila kufuata kanuni na sheria za kuingiza dawa hizo katika maonesho.

Kwa mujibu wa Semwanza, wanakagua dawa na kama wakikuta hazijathibitishwa na TFDA na mamlaka nyingine, wanamuamuru mjasiriamali kuacha kuzitangaza mpaka apate kibali na kuwaasa wanaowaleta wajasiriamali katika maonesho hayo ya kimataifa kuhakikisha wanafuata vigezo.

Wiki iliyopita TFDA, ilionya wananchi dhidi ya matumizi ya dawa za tiba mbadala, zikiwamo zinazokuza maumbile, ambazo bado hazijasajiliwa na Mamlaka hiyo baada ya kuchunguza usalama, ubora na ufanisi wa dawa hizo.

Mamlaka hiyo  ilieleza kuwa, ilitoa nafasi ya watoa tiba mbadala kwenda kusajili dawa zao, lakini mwitiko umekuwa hafifu. 

 

TDFA yenye dhamana ya kusimamia ubora na usalama wa bidhaa za vyakula na dawa, ikiwa ni pamoja na dawa za mitishamba, vipodozi na vifaa tiba vinavyouzwa katika soko la Tanzania, imeeleza kuwa watoa huduma wa tiba mbadala, wengi hawako tayari kubainisha aina ya mchanganyiko wa dawa hizo jambo ambalo ni hatari kwa walaji.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: