MAPACHA WALIOTENGANISHWA INDIA WAISHI KWA SHIDA


Mwezi mmoja baada ya pacha waliokuwa wameungana, Ericana na Eliud kurejea nyumbani mkoani Mbeya baada ya kutenganishwa huko India, imebainika kuwa sasa wanaishi maisha magumu.

Pacha hao ambao habari zao ziliuteka umma, walizaliwa jijini Mbeya, Februari 20, mwaka jana wakiwa wameungana kiunoni na kuwafanya washindwe kuonana sura hadi baada ya upasuaji huo.

Pamoja na furaha ya kuonana sura, Gazeti la The Citizen, limeripoti kuwa pacha hao wamekutana na hali ngumu ya maisha kutokana na uwezo mdogo wa familia yao, ikielezwa kuwa wakati mwingine hata mlo unakosekana.

“Maisha ya sasa si kama ilivyokuwa India ambako walikuwa wanakula vyakula vizuri, wanalala pazuri, hapa ni bahati nasibu hata kupata milo mitatu. Muda mfupi ujao hata unga wao wa uji utakwisha, limebaki kopo moja tu,” alisema baba yao mzazi, Erick Mwakyusa ambaye ni dereva wa bodaboda.

Mwakyusa alisema alipopata taarifa kuwa mke wake atajifungua pacha, alipata wakati mgumu kwani alijua hali ngumu waliyonayo, lakini alichanganyikiwa zaidi baada ya kuambiwa kuwa pacha hao wameungana pia.

“Kulea pacha ni jambo moja, lakini kulea walioungana ni ngumu zaidi, sikujua ni jinsi gani nitawalea katika hali waliyokuwa nayo,” alisema Mwakyusa.

Katika changamoto za kutafuta matibabu, Mwakyusa alisema alipotezana na familia yake wakati mkewe Grace alipokwenda Dar es Salaam kutafuta matibabu na baadaye akapata msaada kwenda India alikokaa kwa miezi tisa.

Mwakyusa ambaye ameikodi pikipiki hiyo kwa ajili ya kufanyia biashara anasema hutakiwa kukabidhi kiasi cha Sh6,000 au 8,000 kwa siku.

Kutokana na udogo wa chumba wanacholala, Mwakyusa na Grace hulazimika kulala chini kwenye godoro na kuwaachia watoto wao wawili kitanda cha futi tatu kwa tano. “Licha ya ugumu huo wa maisha, tunaishukuru Serikali kwa kutusaidia kufika India na kututakia mema,” alisema Mwakyusa.

“Tunalala njaa mara kwa mara, ingawa watoto wametibiwa na ni wazima, lakini bado tuna changamoto za kuwafanya wawe hai,” alisema.

Grace alipoulizwa anataka msaada wa aina gani, alisema, “Ningepata Sh150,000 ningefanya biashara,”

Kutokana na kauli hiyo, Balozi wa Kenya nchini, George Owuor alifika katika Ofisi za Mwananchi na kuahidi kutoa fedha alizohitaji Grace kwa ajili ya biashara na wafanyakazi wa ubalozi huo kukusanya fedha kwa ajili ya kununua bodaboda ya baba wa watoto hao ili aachane na kukodi kwa tajiri.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: