HATIMAYE IKULU YAONYESHA HATI YA MUUNGANO



Baada ya mvutano wa muda mrefu bungeni kuhusu ilipo Hati ya Muungano, Ikulu jana iliamua kuitoa hadharani huku ikisisitiza kuwa, “ni halisi na haikuchakachuliwa.”

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza Ikulu jana, alisema madai ya kuonyeshwa kwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi na hawakufahamu kama yangefika hatua yalipofikia.

“Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo na ilikuwapo siku zote,” alisema Balozi Sefue na kuongeza: “Hata hivyo, tukubaliane kwamba kuna hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, kama Jamhuri huru, kama Muungano huru ambazo zinahifadhiwa kama mboni ya jicho.

Balozi Sefue alizitaja kuwa ni Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962 na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964 na kusema zinahifadhiwa maeneo maalumu ili zisipotee au kuharibika.

“Maneno yamekuwa mengi mno, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi kiasi cha wananchi kuanza kutia shaka kuwa hati ya Muungano ipo au la,” alisema na kuongeza:

“Kutokana na agizo na ridhaa ya Rais Jakaya Kikwete, ninaleta kwenu waandishi wa habari hati halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume ili muione, mridhike nayo na muwajulishe wananchi.”

Baada ya kuwaonyesha aliwagawia wanahabari hao nakala ya hati hiyo na kusema Ikulu itafanya utaratibu wa kuiweka katika makumbusho ya Taifa ili kila mwananchi anayependa kuiona aende huko.

Kuhusu hati hiyo kupelekwa bungeni mjini Dodoma, Balozi Sefue alisema iwapo Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta ataiomba, Ikulu itaipeleka ili kuondoa mjadala wa uwepo wa hati hiyo.

“Tumesikitishwa, kusononeka na kufadhaika sana na tuhuma nzito kwamba waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia Watanzania wenzetu wafikie hapo ni jambo zito,” alisema Balozi Sefue

Katika kipindi cha maswali, Balozi Sefue alishindwa kubainisha ilikuwa wapi wakati wote na kusisitiza: “Kazi ya leo ilikuwa ni kuwaonyesha hati hiyo na ninaomba maswali yenu yajikite katika hili.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: