BUNGE LA KATIBA-POSHO WANAZOTAKA ZAPINGWA KILA KONA


Wakati maombi ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya kuongezewa posho yakipingwa kila kona, uongozi wa muda wa Bunge hilo umeunda kamati kuchunguza uhalali wa maombi hayo.

Juzi, ndani ya kikao cha Bunge hilo, baadhi ya wajumbe walieleza mahitaji yao ya posho kuongezwa wakisema kiwango cha Sh300,000 (Sh80,000 za kujikimu na Sh220,000 kwa kikao), hakitoshi.

Baada ya maombi hayo, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho aliahidi kuliwasilisha suala hilo serikalini ili lifanyiwe kazi, lakini jana aliamua kuunda timu ya wajumbe sita kuchunguza uhalali wa posho hizo.

Posho kupingwa

Baadhi ya vyama vya siasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida wameshangazwa na maombi hayo ya posho, wakisema wajumbe wamesahau kilichowapeleka bungeni na kukimbilia kutetea masilahi yao.

Vyama vya Chadema na CUF kwa nyakati tofauti, vilisema kuwa vitaanzisha juhudi za kuwataka wabunge wao ambao ni wajumbe wasusie agenda yoyote inayotaka kuongezwa kwa posho hizo.

Tamko la vyama hivyo limetolewa huku Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho wajumbe wake ndio wanaodaiwa kupigia debe mpango huo, kikisema kitatoa ufafanuzi juu ya hoja hizo baada ya kupata ‘taarifa rasmi’.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema jana kuwa wajumbe hao hawakupaswa kudai nyongeza ya posho kwa vile hawakutumwa kwenda Dodoma kudai marupurupu ya fedha.

Alisema kuanza kujadili suala la nyongeza ya posho badala ya kuzungumzia hoja za msingi zilizopo kwenye Rasimu ya Katiba, ni sawa na kuwapuuza wananchi ambao wanasubiri kupata Katiba Mpya.

“Wametoka kwenye hoja na kutupeleka kwenye mambo mengine ambayo hayana msingi wowote. Sisi kama Chadema tunapinga na tunataka wabunge wetu watambue hilo,” alisema.

Alisema wale wanaolalamika kwamba Sh300, 000 hazitoshi wanajaribu kupindisha ukweli, kwani kuna baadhi ya watumishi wa Serikali wanalipwa kiasi hicho ikiwa ni mshahara wao wa kila mwezi.

Alisema Chadema kimewataka wabunge wake kutojiingiza kwenye malalamiko hayo badala yake wazingatie kile walichotumwa na wananchi kwenda Dodoma.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: