ASKARI MAGEREZA WADAIWA KUUWA MFUNGWA



Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Omary Mtiga
Askari Magereza wanane, wamefikishwa mahakamani wilayani Mafia mkoani Pwani kwa tuhuma za mauaji ya mfungwa.

Mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Wilaya ya Mafia, Hassan Makube, ilidaiwa kuwa, Desemba 19 mwaka jana, askari hao walimuua Basiri Makungu aliyekuwa akitumikia kifungo katika Gereza la Kilombero, lililopo kwenye wilaya hiyo. Askari waliofikishwa mahakamani hapo walitajwa kuwa ni Sajenti Sadick na wenzake ambao walifunguliwa kesi namba 1/2014.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja walimuua Makungu, baada ya kumshambulia kwa kipigo mwishoni mwa mwaka jana.

Kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu, pamoja na kesi ya mauaji kutokuwa na dhamana, watuhumiwa hao walirudishwa rumande hadi Februari 7 mwaka huu.

Akizungumzia tukio hilo, ofisa wa juu wa Jeshi la Magereza, Menrad Tesha alisema kuwa, jeshi hilo linafahamu taarifa za askari hao kushtakiwa kwa makosa hayo, lakini akasema suala hilo halipo chini yao. Tesha alipohojiwa kuhusu mustakabali wa ajira za askari hao na iwapo wanashtakiwa kama raia au wafungwa alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa sasa.

“Siwezi kuzungumzia ajira zao hapa, huu siyo utendaji unaotakiwa, kila kitu kina taratibu zake, hivyo siwezi kulizungumzia hilo,” alisema Tesha.

Alieleza kuwa askari anapotuhumiwa kwa makosa yoyote suala lake huachwa mikononi mwa vyombo vinavyostahili, ili kuwachukulia hatua.

“Hivi sasa wale ni watuhumiwa, kwa hiyo mimi kuliongelea siyo sahihi. Kama kuna kitu ungetaka kufahamu, basi nakushauri mfuate mkuu wa gereza kule walipo sasa (Mafia), atakueleza kila unachotaka kufahamu kuhusu askari hao kwani bado wapo huko,” alisema Tesha.

Matukio ya Askari Magereza kuua wafungwa

Februari mwaka jana ilidaiwa kuwa Willfred Mallya mwenye namba 315 aliyefungwa mwaka 2003 katika katika Gereza la Kisongo mjini Arusha aliuawa kutokana na kipigo cha Askari Magereza.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Omary Mtiga licha ya kukiri kutokea kwa kifo cha mfungwa huyo, alikanusha kuwa kilitokana na kipigo cha askari hao akisema kifo chake kilikuwa ni cha kawaida.

Desemba mwaka 2010, askari wanne wa jeshi hilo waliokuwa wakifanya kazi katika Gereza la Lilungu mkoani Mtwara, walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji ya mfungwa.

Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Abdulhaman Mohamed mbele ya Hakimu Stepheni Mbungu.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Oktoba 31, mwaka 2010 watuhumiwa hao kwa pamoja walimuua mfungwa aliyekuwa na namba 215, Kasimu Kumchaya.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: