MKURUGENZI EROLINK ATOROKA NCHINI


MKURUGENZI wa Kampuni ya uwakala wa ajira ya Erolink Tanzania Limited ametoroka nchini baada ya serikali kubaini kuwa ameikosesha kodi ya zaidi ya sh bilioni tatu kwa miaka mitatu.

Tanzania Daima imedokezwa kuwa mkurugenzi huyo ajulikanaye kwa jina la Elvis Rogers Kamanyile, aliondoka nchini na familia yake kuhofia hatua za kisheria ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa kosa la kukwepa kodi.

Aidha, chanzo chetu kilidokeza kuwa mkurugenzi huyo aliondoka nchini kwa madai ya kwenda kutibiwa ingawa madai hayo yanasemekana kutokuwa na ukweli ndani yake. Habari zilizopatikana zilidokeza kuwa hivi sasa kampuni hiyo ya Erolink ipo katika mchakato wa kubadili jina ili kuepuka kesi ya madai ya kukwepa kodi inayokuja mbele yake, huku baadhi ya viongozi serikalini (majina yanahifadhiwa) wakiwa mstari wa mbele kufanikisha zoezi hilo.

“Hivi sasa Erolink ipo katika mchakato wa kubadili jina ili kupoteza ushahidi lakini pia kama hiyo haitoshi zoezi hilo linasimamiwa na baadhi ya viongozi wazito serikalini, kutokana na baba wa mkurugenzi huyo aliwahi kuwa mkurugenzi wa moja ya benki kubwa hapa nchini ili kuhakikisha sakata hilo linazimika kwa sheria kutofuata mkondo wake,” kilisisitiza chanzo hicho.

Hofu ya mkurugenzi huyo inakuja baada ya agizo la Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alilolitoa wiki mbili zlizopita la kupiga marufuku utaratibu wa mawakala kuajiri wafanyakazi wanaowatafutia.

Badala yake aliwataka mawakala husika wakiwamo Erolink kuwahamisha wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwao na mawakala wengine kwenda kampuni husika moja kwa moja na kuwa waajiri halali katika kipindi cha mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa Waziri Kabaka, kuhusiana na uchunguzi uliofanywa kwa kampuni 13 ulibaini kuwepo kwa ujanja unaotumiwa na mawakala wanane kutofuata na kuzingatia sheria na taratibu ambapo mwisho wake hukwepa kodi na kujipatia faida kwa kutotoa haki za msingi kwa wafanyakazi kama inavyofanywa na Erolink.

Mbali ya hayo, uchunguzi pia ulibaini kutokuwapo kwa tahadhari kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huo ikiwemo kukosa haki za kijamii kama likizo ya uzazi, matibabu na sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii.

Waziri Kabaka alibainisha kuwa uwepo wa kampuni za mawakala wanaoajiri watu unaleta mfumo wa kibaguzi katika mishahara kwa kazi za aina moja, kukosa fursa ya kujiendeleza kielimu na mafunzo, kukosekana kwa uasalama na uhakika wa ajira huku wafanyakazi wakilipwa mishahara ya kima cha chini kinyume cha sekta wanayofanya kazi.

Hata hivyo kampuni nyingi za uwakala hapa nchini ikiwamo Erolink zinakiuka sheria ya ajira na uhusiano kazini namba 6/2004 inayomtaka mwajiri kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha wafanyakazi bila kujali jinsia zao wanalipwa mshahara linganifu kwa kazi zenye uzito na thamani sawa.

Pamoja na katazo hilo Tanzania Daima limebaini kuwapo kwa wafanyakazi wa kigeni wanaohusishwa katika utaratibu wa kukodishwa ambao Waziri Kabaka aliwataka kuhakikisha wanaomba vibali huku akisisitiza kwamba waajiriwe na kampuni zinazowakodisha.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: