MAFURIKO YATIKISA JIJI LA DAR..HALI NI MBAYA


MVUA zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha uharibufu wa miundombinu ya barabara, nguzo za umeme na mingine kuharibika, hali iliyokwamisha shughuli nyingi jana.

Mvua hizo zilizonyesha usiku mzima wa kuamkia jana, ziliambatana na upepo mkali, radi na ngurumo nzito zilizowatia hofu wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam.

Wakazi waishio mabondeni walikuwa na kazi ya ziada kwani wengi nyumba zao ziliingia maji na kusababisha baadhi yao kuhama makazi yao usiku, huku wengine wakipoteza vitu  na samani mbalimbali.

Kutokana na barabara za Jiji la Dar es Salaam kufurika maji, askari wa Usalaama Barabarani (Trafiki), walikuwa na kazi ya ziada kuyaruhusu magari kupita njia ambazo ziko salama bila kujali sheria.

Tanzania Daima ilishuhudia barabara kuu zote na maeneo mengine kufurika maji na kusababisha wakazi wa jiji hilo kupita kwa shida.

Aidha, baadhi ya wakazi  waliokuwa wakitoka Pugu, walilazimika kupanda magari ya kubeba ng’ombe yaliyokuwa yakitokea mnadani baada ya daladala nyingi kusitisha safari zake.

Wakati hali ikiwa hivyo, eneo la Jangwani maji hayo  yalizoa miundombinu ya mabomba ya maji ikiwemo yale yaliyojengwa hivi karibuni kupisha ujenzi wa barabara ya magari yaendayo haraka (DART).

Pia kulikuwa na baadhi ya vijana katika eneo hilo waliokuwa wakijiokotea vitu mbalimbali vilivyokuwa vikielea juu ya maji.

Akizungumzia kufurika kwa maji kwenye barabara hizo kuu, Sajenti James Walter, alisema ilibidi kuyaruhusu magari ya abiria yapite njia nyingine kinyume cha  sheria, lengo likiwa kuwafikisha salama abiria kule wanakokwenda.

“Kwa kweli hali ni mbaya lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha abiria na watumiaji wa barabara hizi hawakwami njiani,” alisema Walter.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments: